emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

ZUHURA MWINDI: MFANYAKAZI BORA WA e-GA MWAKA 2024


ZUHURA MWINDI: MFANYAKAZI BORA WA e-GA MWAKA 2024


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imemtangaza Msaidizi wa Mtendaji Mkuu Bi. Zuhura Mwindi, kuwa mfanyakazi bora wa Mamlaka kwa mwaka 2024, baada ya kuibuka mshindi kwa kupata kura nyingi dhidi ya washindani wengine.

Uchaguzi wa mfanyakazi bora wa Mamlaka ulifanyika April 25 mwaka huu, baada ya kuwashindanisha wafanyakazi bora 10 kutoka katika Idara na vitengo na kisha Menejimenti kupiga kura ili kumpata mfanyakazi bora wa Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Akizungumza wakati wa zoezi la uchaguzi, Meneja Rasilimaliwatu na Utawala Bw. Erick Kalembo alisema kuwa, orodha ya wafanyakazi bora wa Idara na Vitengo ilipatikana baada ya kufanyika uchaguzi wa ndani kwa kila Idara na vitengo na kisha orodha hiyo kuwasilishwa Idara ya Huduma na Uwezeshaji.

“Tumepokea orodha ya wafanyakazi bora kutoka kila Idara na Vitengo ambapo watumishi wa maeneo husika walipiga kura huru na sasa ni wakati wa sisi Menejimenti kupiga kura ili tuweze kumpata Mfanyakazi bora wa taasisi ”, alisema Bw. Kalembo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mha. Benedict Ndomba, alisema kuwa e-GA inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wake wote katika kufikia malengo ya taasisi na kuwa, uchaguzi wa mfanyakazi bora ni motisha kwa wafanyakazi wote kuendelea kufanya kazi vizuri zaidi na kwa weledi..

“Watumishi wote wa e-GA ni bora na ndiomaana taasisi huweza kufikia malengo iliyojiwekea kila mwaka kwa mujibu wa mpango mkakati wa Mamlaka wa mwaka 2021/2022 – 2025/2026 kwani kila mtumishi hufanya kazi kwa bidii, hivyo niwapongeze sana watumishi wote wa e-GA” alisema Ndomba.

Aidha, Ndomba aliitaka Menejimenti kuwapima watumishi wote bora waliochaguliwa kwa kila Idara na Vitengo na kisha kupiga kura kwa uwazi na kumchagua mfanyakazi bora wa Mamlaka, kwa kuzingatia vigezo vilivyopo bila upendeleo wa aina yeyote.

Uchaguzi huo ulifanyika kwa njia ya mtandao ‘online’ kupitia Mfumo wa Kidijitali wa uendeshaji vikao wa e-Mikutano ambapo Menejimenti ilipiga kura na kupata wafanyakazi bora watatu (3) walioingia tatu bora na hatimaye kumpata mfanyakazi bora wa taasisi.

Walioingia tatu bora ni Bi. Zuhura Mwindi aliyeshika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Afisa TEHAMA Darwin King'ani kutoka Idara ya Huduma za TEHAMA na Afisa TEHAMA Stanslaus Kayombo kutoka Idara ya Miundombinu na Uendeshaji aliyeshika nafasi ya tatu.

Naye Mfanyakazi bora wa Mamlaka kwa mwaka 2024 Bi. Zuhura Mwindi, aliishukuru Mamlaka kwa kumchagua na kutambua jitihada zake katika utendaji kazi na kwamba ushindi huo umeongeza chachu ya kufanya kazi kwa ufanisi na bidii zaidi.

Aidha, Bi. Zuhura aliwashukuru watumishi wa Idara ya Huduma za Uendeshaji kwa ushirikiano na kutambua mchango wake katika Idara uliopelekea kuibuka mshindi wa Idara hiyo na hatimaye kuwa mfanyakazi bora wa taasisi.

“Ninaishukuru sana Menejimenti na watumishi wenzangu wa e-GA kwa kutambua na kuthamini jitihada zangu, niwatie moyo watumishi wenzangu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kujituma ili kuweza kufikia malengo ya Taasisi” Alisema Bi. Mwindi.