Wakaguzi wa Ndani katika taasisi na mashirika ya umma wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika ukaguzi wa miradi na mifumo ya TEHAMA ili kulinda thamani halisi ya fedha za Serikali katika miradi hiyo.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi anayeshughulikia Wizara, Idara zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali, kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (IAG) Bw. Paison Mwamnyasi, wakati akifungua mafunzo ya awamu ya saba kuhusu Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Wakaguzi wa Ndani wa Serikali yanayofanyika mkoani Morogoro.
Alisema kuwa, lengo la mafuinzo hayo ni kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani katika ukaguzi wa mifumo na miradi mbalimbali ya TEHAMA Serikalini, ili kuhakikisha miradi na mifumo yote ya TEHAMA katika taasisi za umma inazingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kuanzia hatua za awali hadi za mwisho za ujenzi wa miradi hiyo.
“Wakaguzi wa Ndani mnapaswa kuhakikisha kuwa taasisi zenu zinazingatia matakwa ya kisheria katika Miradi na Mifumo ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na miradi hiyo kuwasilishwa e-GA ili kupata kibali kabla ya kuanza utekelezaji wake”, alisema Bw. Mwamnyasi.
Alisisitiza kuwa, kaguzi zote za mifumo zinapaswa kufanyika kwa vitendo na sio kwa nadharia na hivyo, ni wajibu wa Maofisa hao kuwa na uelewa kuhusu Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao ili waweze kufanya kaguzi za mifumo ya TEHAMA kwa ufanisi na weledi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Sylvani Shayo, alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani ili kuongeza ufanisa katika utendaji kazi wao na kushiriki katika ujenzi wa Serikali Mtandao.
“Tunatarajia kuwa, baada ya kupata mafunzo haya, Wakaguzi wote wa Ndani mliopo hapa mtakuwa mabalozi wazuri wa Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao na mtatoa ushauri chanya wenye tija katika taasisi zenu ili kwa pamoja tuweze kuijenga Serikali Mtandao”, alisema Bw.Shayo.
Mafunzo hayo ya siku nne yameratibiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (IAG) yanalenga kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani katika kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha zaidi ambapo jumla ya Wakaguzi wa Ndani 70 kutoka taasisi na mashirika ya umma 49 wanapata mafunzo hayo.