Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Seif Shekalaghe, amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA ya kutolea huduma za afya inakidhi matakwa ya Sheria na viwango vya Serikali Mtandao.
Dkt. Seif alitoa kauli hiyo juzi jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Umahiri katika masuala ya afya ya Kidigitali (CDH), ambacho kinalenga kuhakikisha utoaji wa huduma za afya kidijitali unaimarika ili kumrahisishia mwananchi kupata huduma hizo kwa haraka zaidi mahali alipo.
Alifafanua kuwa, Wizara hiyo imedhamiria kuhakikisha mifumo yote ya afya inasomana kwa wakati mmoja ili kuweza kuboresha huduma za afya na kuwataka wataalamu wa TEHAMA katika Wizara hiyo kukitumia vema kituo hicho ili kufikia malengo ya Wizara ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya kidijitali.
“Kupitia kituo hiki, Wizara inataka kuona huduma za afya zinaimarika na taarifa zote za afya kutoka hospitali zote zinasomana kwa wakati mmoja ili kila muhusika aweze kuona kwa wakati, lakini pia kiongozi yeyote anayetaka kufahamu idadi ya madaktari bingwa hahitaji kukupigia simu bali anachotakiwa ni kuingia tu kwenye mfumo na kupata taarifa za wakati huo”alisema.
Aliongeza kuwa, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imekuwa na ushirikiano mkubwa kwa Wizara hiyo kwenye eneo la TEHAMA katika kuhakikisha mifumo iliyopo inapungua na kuwa na mifumo michache inayobadilishana taarifa, hali ambayo itasaidia kwa kikubwa kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji kazi katika Wizara na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alisistiza kuwa, kituo hicho kitumiwe kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Serikali Mtandao ili kuhakikisha wataalamu wazawa wanatumia vema ujuzi wao katika mazingira mazuri zaidi ili kutengeneza mifumo ya TEHAMA yenye tija kwa Serikali na wananchi katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya kidijitali.
Mwakilishi wa e-GA ambaye pia ni Meneja Udhibiti wa viwango vya Serikali Mtandao Bi. Sultana Seiff, alisema kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ili kuhakikisha mifumo ya TEHAMA inayotumika katika sekta ya afya inakuwa thabiti na salama ili kuongeza ufanisi.
Alisisitiza kuwa, Mamlaka itahakikisha mifumo yote ya sekta ya Afya inakidhi viwango vya Serikali Mtandao vilivyowekwa lakini pia inazingatia usiri wa taarifa za wagonjwa na usalama wao, ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuhakikisha huduma za afya zinaboreka na kumrahisishia mwananchi kupata huduma hizo mahali alipo bila kukiuka maadili ya utendaji kazi katika sekta hiyo kwa kuzingatia sheria, sera na miongozo ya kiafya.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA Wizara ya Afya Bw. Silvanus Ilomo alisema kituo hicho sio kwa ajili ya Wizara ya Afya pekee hivyo mlango uko wazi kwa Wizara na taasisi mbalimbali za umma kutumia kituo hicho ili kuhakikisha jitihada za Serikali Mtandao nchini zinaimarika katika sekta zote za umma.