Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. George Simbachawene, amewataka watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu na uadilifu, ili kuhakikisha dhamira ya ujenzi wa Serikali Mtandao inatimia.Waziri Simbachawene ameyasema hayo jana baada ya kutembelea Ofisi za e-GA kituo cha Iringa na kufanya mazungumzo na watumishi wa kituo hicho.
Amebainisha kuwa, dhamira ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ni kuona huduma kwa wananchi zinakuwa bora na kupatikana kwa urahisi zaidi kupitia TEHAMA.
“Wengi wenu hapa ni vijana wadogo, tuna imani kubwa nanyi katika kuhakikisha ufanisi wa utendaji kazi Serikalini unaimarika na wananchi wanapata huduma kwa urahisi na gharama nafuu mahali walipo kwa njia ya kidijitali, hivyo muendelee kuwa wabunifu lakini uadilifu uwe ngazi yenu katika kuisaidia Serikali kwenye mageuzi haya”, amesema Simbachawene.
Katika ziara hiyo Waziri Simbachawene ameongozana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete katika ziara hiyo fupi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mha. Benedict Ndomba, amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kutembelea kituo hicho na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa kituo hicho