Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (Mb) ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kuziwezesha Taasisi za Umma kutumia Mifumo ya TEHAMA ambayo imesaidia kuboresha utendaji kazi ndani ya Taasisi hizo pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri Mhagama aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa uzinduzi rasmi wa Mfumo wa Usimamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja - (Collective Investment Schemes) unaojulikana kama FAS (Funds Administration System) uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC)jijini Dar Es Salaam.
“Naipongeza sana Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuziwezesha Taasisi za Umma kutumia Mifumo ya TEHAMA inayoboresha utendaji kazi, niiombe e-GA kuhakikisha kuwa Taasisi zote za Umma zinafanya kazi zake kidijitali ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Taasisi hizo”, alisema Mhe. Mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama alisema kuwa Taasisi hizi mbili za Watumishi Housing na Mamlaka ya Serikali Mtandao zimeshirikiana katika kubuni, kusanifu na kutengeneza Mfuko wa pamoja wa Uwekezaji (Faida Fund), unaowasadia wananchi wa hali ya chini, kati na juu kupata fedha kupitia uwekezaji wa pamoja.
Vile vile, Mhe. Mhagama alisema kuwa juhudi za e-GA zimesaidia katika kubuni, kusanifu na kusimamia Mfumo wa Uendeshaji Mfuko wa Faida Fund kwa kutumia gharama ndogo naunasaidia watanzania wote kuwekeza na kujiwekea akiba mahali popote walipo.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. Deogratius John Ndejembi (Mb) ameipongeza e-GA kwa kubuni, kusanifu na kutengeneza Mifumo inayosaidia Taasisi za Umma kutekeleza majukumu yake kwa urahisi na ufanisi.
Mhe. Ndejembi ameitaka e-GA kuendelea kuzisaidia bila kuchoka Taasisi nyingine za Umma katika kuzijengea uwezo ili ziweze kutekeleza na kujenga Serikali Mtandao ili kutimiza azma ya Serikali ya Kidijitali.
Akielezea taarifa ya Mfumo wa Uendeshaji Mfuko wa Faida Fund, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi. Benedict Ndomba alisema kuwa Mfumo huu unamwezesha Mwekezaji kuchagua njia mojawapo kati ya njia tatu za kutumia kununua au kuuza vipande.
“ Njia ya kwanza ni ya Mtandao (Web Application) kwa kubofya www.fas.whi.go.tz, njia ya pili ni kupitia simu za kiganjani ambayo hutumiwa na watumiaji wote wenye simu za kiganjani kwa kubofya namba ya Huduma za Serikali *152*00# na kuchagua namba 1 malipo kisha namba 6 WHI na kufuata maelekezo kadiri ya hitaji la mtumiaji, na njia ya tatu ni kwa watumiaji wa simu janja kwa kupakua aplikesheni ya Faida Fund App kwa watumiaji wa Android, na kujaza taarifa zote kwa usahihi ikiwa ni pamoja na namba ya simu ili aweze kupokea namba ya malipo atakayotumia kulipa wakati wa kununua vipande na kufuatilia mwenendo wa uwekezaji”, alisema Ndomba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa WHI Dkt. Fred Msemwa aliishukuru e-GA kwakuwa na watumishi wenye weledi na ubunifu mkubwa ambao wameiwezesha WHI kupata matokeo chanya kupitia Mfumo wa Uendeshaji Mfuko wa Faida Fund.
Mfumo wa Usimamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja - (Collective Investment Schemes) unaojulikana kama FAS (Funds Administration System) unalenga kusimamia uwekezaji katika Mfuko wa FAIDA ujulikanao kama FAIDA FUND.
Mfumo huu ni wa kwanza kutengenezwa hapa nchini na umetengenezwa kwa kutumia wataalamu wazawa kuanzia hatua ya mwanzo hadi ya mwisho ya ujenzi.