emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WAZIRI BASHE AZINDUA MFUMO WA MUVU


WAZIRI BASHE AZINDUA MFUMO WA MUVU


Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe, amezindua Mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU) unaowezesha na kurahisisha uhamasishaji, usimamizi na uendeshaji wa Vyama vya Ushirika kidijitali.

Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni wakati wa kilele cha maadhisho ya siku ya ushirika duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Nanenane Ipuli Mjini Tabora, na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi pamoja na waandishi wa habari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe.Bashe alisema mfumo wa MUVU utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikabili sekta ya Ushirika kwa muda mrefu ikiwemo changamoto ya soko la mazao ya wakulima.

“Kupitia mfumo huu, wakulima hawatadhulumiwa tena mazao yao kwakuwa mkulima atapata taarifa ya kila hatua kupitia simu yake ya kiganjani na kumuwezesha kujua masoko ya mazao yake”, alisema Mhe.Bashe.

Vilevile, Mhe.Bashe aliipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana kikamilifu na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) katika kujenga na kusanifu mfumo huo kuanzia hatua ya awali mpaka kukamilika pamoja na usimamizi wa mfumo huo.

Aidha, alisisitiza mfumo huo kutumika katika mazao yote ikiwemo zao la pamba na tumbaku na kuitaka e-GA kuhakikisha mfumo huo unawasiliana na mfumo wa kusajili wakulima wa nchi nzima, sambamba na kuwa na mfumo mmoja ambao utamsajili mkulima na kuonesha miamala yake ya kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu e-GA, Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA e-GA, Bw. Ricco Boma alisema katika mwaka wa fedha 2023/24 e-GA imejipanga kujenga Mfumo mkuu wa sekta ya kilimo wenye dirisha moja tu kwa Mkulima, msambazaji wa pembejeo na mfanyabishara wa Kilimo yaani ‘Agriculture Single Window’, mifumo mingine itakuwa ni mifumo saidizi yaani ‘backend supporting systems’ itakayokuwa inazungumza na mfumo mkuu wa Kilimo.

‘’Mfumo huu utakuwa umebeba mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, hivyo basi ninaomba kutoa wito kwa wadau wa sekta ya kilimo kuunga mkono juhudi hizi na kutoa ushirikiano ili Mamlaka ya Serikali Mtandao iweze kutekeleza agizo la Mhe Rais na Sheria ya Serikali Mtandao inayoitaka Mamlaka kutengeneza mifumo michache inayowasiliana’’ Alisema Bw.Ricco

Naye Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania Dkt. Benson Ndiege, alisema zoezi la utengenezaji wa mfumo limekamilika na tayari vyama vya ushirika vinaendelea na usajili, na kuanzia sasa vyama vyote vya Ushirika vitahitajika kutoa taarifa zake kupitia mfumo wa MUVU.