emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WATUMISHI WA e-GA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA


WATUMISHI WA e-GA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA


Afisa Uchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Dorothea Mrema, amewataka watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuzingadia uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Bi Dorothea alitoa kauli hiyo Januari 6 mwaka huu, wakati akitoa elimu kuhusu rushwa mahala pa kazi kwa watumishi wa e-GA, kwenye mkutano wa watumishi hao uliofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa, watumishi wa umma wanapaswa kushiriki mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa TAKUKURU, pale wanaposhuhudia uwepo wa viashiria au vitendo vya rushwa katika maeneo mbalimbali ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

“Kila mtumishi ana wajibu wa kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa mahali pa kazi ili kuhakikisha jitihada za Serikali zinazofanywa dhidi ya mapambano ya rushwa zinafanikiwa na kuhakikisha rasilimali za taifa pamoja na fedha za umma zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa na kuleta tija kwa taifa”, alisisitiza.

Aliongeza kuwa, TAKUKURU inatambua mchango wa TEHAMA katika kuzuia rushwa ikiwa ni pamoja na uwepo wa mifumo mbalimbali ya kielektroniki ya utoaji wa huduma kwa wananchi, ambayo imechangia kuimarisha utoaji wa huduma na kupunguza mianya ya rushwa.

“Tunaipongeza e-GA kwa kutengeneza mifumo mbalimbali ya kielektroniki inayorahisisha utendaji kazi wa serikali na utoaji wa huduma kwa umma, lakini pia mifumo hii imesaidia kupunguza mianya ya rushwa kwa asilimia kubwa tofauti na awali”, alifafanua Bi. Dorothea.

Alibainisha kuwa, ni vema kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu uwepo na upatikanaji wa huduma za Serikali kupitia mifumo ya kielektroniki iliyopo sambamba na kuendelea kuiboresha zaidi ili wananchi waweze kupata huduma bora na kuondoa mianya yote ya rushwa.

Aidha, Bi. Dorothea ametoa rai kwa wanachi ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma na wanafunzi, kujiunga katika vikundi (klabu) mbalimbali za mapambano dhidi ya rushwa ili kupata uelewa zaidi na kufahamu mikakati mbalimbali itakayosaidia katika kuondoa rushwa nchini.