Wanawake nchini, wametakiwa kutumia vema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuongeza vipato vyao na kukuza pato la taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na watumishi wanawake wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Machi 8, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo kitaifa yalifanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali wilayani Chamwino jijini Dodoma.
Meneja wa Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao Bi. Sultana Seiff alisema kuwa, kwakuwa TEHAMA ni nyenzo wezeshi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ni vema wanawake wakatumia fursa mbalimbali zitokanazo na TEHAMA ili kujiimarisha kiuchumi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
“Nawasisitiza wanawake wenzangu kutumia TEHAMA katika shughuli zao za kijamii ili kuboresha uchumi wao, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wao na kuleta tija kwa taifa kwakuwa TEHAMA inatoa fursa nyingi za kiuchumi hivyo ni vizuri tukatambua fursa hizo na kuzitumia kikamilifu kwa ajili ya maendeleo yetu na taifa kwa ujumla”, alisisitiza Bi. Sultana.
Kwa upande wake Afisa TEHAMA wa e-GA Bi. Ndili Yusuph alisema kuwa, Mamlaka inatambua mchango wa wanawake kwenye ujenzi wa Serikali ya kidijiti, katika nyanja mbalimbali ikiwemo ulinzi wa mtandao, utengenezaji na uchambuzi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA hivyo ni muhimu wanawake wakatumia fursa hiyo kujifunza TEHAMA.
Aliongeza kuwa, kwa sasa dunia ipo katika mapinduzi ya uchumi wa kidijitali ambapo TEHAMA ni nyenzo kuu na inatoa fursa nyingi ambazo wanawake hawana budi kushiriki ili kuisadia nchi yetu iweze kufanikiwa na kupiga hatua katika mapinduzi hayo.
“Nitoe rai kwa wanawake wenzangu hasa wale waliopo shuleni na kazini kujifunza taaluma mbalimbali za TEHAMA ili tuweze kushiriki moja moja katika kukuza jitihada za Serikali Mtandao na vilevile kujiimarisha kiuchumi katika ngazi za familia na jamii zetu”, alifafanua Bi. Ndili.
Naye Afisa TEHAMA wa e-GA Bi. Halima Husein, aliwapongeza wanawake wote nchini kwa kuendeleza na kushiriki katika kukuza na kuimarisha jitihada mbalimbali za TEHAMA ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa jamii na kuongeza chachu ya utendaji kazi.
“Wanawake wote tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo katika TEHAMA ili kuhakikisha tunaisaida Serikali kuboresha utendaji wake wa kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi”, alisisitiza Bi. Halima.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 08 kila mwaka ambapo mwaka huu maadhimisho hayo yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Wekeza kwa wanawake: Harakisha maendeleo.”