emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

​​Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao


​​Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao


Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao katika kusanifu miradi ya TEHAMA ili kuhakikisha inaleta tija katika sekta ya kilimo.

Wito huo umetolewa leo na Afisa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw.George Bagomwa, wakati akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa miradi ya TEHAMA Serikalini, kwenye kikao kazi cha Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Alisema kuwa, uzingatiaji wa Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika uanzishwaji wa miradi ya TEHAMA, kutasaidia taasisi hizo kupata ushauri wa kitaalamu kutoka e-GA katika hatua za awali za uanzishwaji wa miradi hiyo na hivyo kuweza kuufanyia kazi ushauri utakaotolewa na e-GA.

"Ni vyema tukafuata matakwa ya Sheria ya Serikali Mtandao, Kanuni zake, Viwango pamoja na Miongozo ili mradi wowote wa TEHAMA mtakauanzisha uweze kuleta manufaa kwa wakulima nchini", alisema Bw. Bagomwa.

Aidha, katika kikao hicho e-GA inatarajia kutoa maelekezo kuhusu uanzishwaji wa kanzidata maalumu za wakulima na wadau wa kilimo.

Kikao hicho cha siku nne kinafanyika mjini Iringa kuanzia tarehe 19 hadi 22 Disemba, pamoja na uwasilishwaji wa mada mbalimbali, kikao hicho kitajadili Dira ya Taifa 2050 na Uelekeo wa Mifumo ya TEHAMA katika sekta ya kilimo.