emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WAKUU WA TAASISI ZA UMMA WATAKIWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UTEKELEZAJI WA SERIKALI MTANDAO


WAKUU WA TAASISI ZA UMMA WATAKIWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UTEKELEZAJI WA SERIKALI MTANDAO


Wakuu wa Taasisi za Umma wametakiwa kuweka mazingira mazuri na wezeshi ya utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA katika taasisi zao ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia yanayoibuka mara kwa mara.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. Ridhiwani Kikwete (Mb), wakati akifunga Kikao Kazi cha Nne cha Serikali Mtandao Februari 08, mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.

Alisema kwamba, kwakuwa dunia inashuhudia ukuaji na mabadiliko ya teknolojia mara kwa mara, ni lazima Maafisa TEHAMA wapate elimu kuhusu teknolojia mpya kadri zinavyoibuka, ikiwa ni pamoja na namna teknolojia hizo zinavyoweza kuimarisha ulinzi wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA Serikalini ili kuhakikisha usalama wa taarifa za Serikali wakati wote.

“Pamoja na kupata elimu mara kwa mara, ni lazima pia Maafisa TEHAMA katika taasisi zote za umma waendeleze ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kupitia msaada na ushauri wa kiufundi unaotolewa na e-GA, ili sote twende pamoja katika kuijenga Serikali ya Kidijitali”, alisema Ridhiwani na kuongeza,

“Nafahamu kuwa, mmetumia kikao hiki cha siku tatu kujadili changamoto za utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, mmejadiliana pia juu ya mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo na mwisho kabisa mkaweka maazimio, niwapongeze sana na kuwaahidi kuwa, Wizara tumeyapokea maazimio na ushauri mlioutoa na tutaweka mpango mkakati wa kufuatilia utekelezaji wake”.

Alibainisha kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria ili e-GA iendelee kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.

“Tutakapokuwa tunatekeleza jitihada mbalimbali za Serikali Mtandao katika taasisi zetu, tuhakikishe pia tunazingatia Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao iliyopo na inayoendelea kutolewa au kuboreshwa mara kwa mara ili kuwa na matumizi salama na sahihi ya TEHAMA Serikalini”, alisisitiza Ridhiwani.

Sambamba na hilo, Ridhiwani aliwataka viongozi wa Taasisi za Umma kutatua changamoto za kiutawala zilizo ndani ya uwezo wao ili kuhakikisha watumishi wote wanakuwa katika mazingira salama na rafiki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi, aliipongeza e-GA kwa jitihada kubwa inazofanya katika kuimarisha na kukuza matumizi ya TEHAMA Serikalini.

“Kukutana kwa wadau mbalimbali katika kikao kazi hiki kutoka katika Wizara, Taasisi na Mashirika ya Umma, ni moja ya jitihada za e-GA za kukuza Serikali Mtandao kwani, wadau wote mmeweza kukutana kwa pamoja na kujadiliana kuhusu hali ya utekelezaji wa Serikali Mtandao, changamoto na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo”, alisema Bw. Xavier.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mha. Benedict Ndomba, aliwashukuru washiriki wa kikao hicho na kuwataka kuhakikisha miradi na mifumo ya TEHAMA inayojengwa katika Taasisi zao inazingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao.

“Lengo ni kuhakikisha miradi na mifumo yote ya TEHAMA katika taasisi zetu inarahisisha utendaji kazi, inaboredha utoaji wa huduma kwa umma na kuwezesha mifumo hiyo kusomana na mifumo mingine ya Serikali na kubadilishana taarifa kwa usalama pindi itakapohitajika kufanya hivyo”, alisisitiza Ndomba.

Kikao kazi hicho kilichoanza Februari 06 na kuhitimishwa Februari 08 mwaka huu kilibeba kaulimbiu isemayo “Uzingatiaji wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Ubadilishanaji Salama wa Taarifa”.