emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

​WAKUU WA IDARA NA VITENGO VYA TEHAMA SERIKALINI WAASWA KUWASHIRIKISHA WAKAGUZI WA NDANI KATIKA UJENZI WA MIFUMO YA TEHAMA


​WAKUU WA IDARA NA VITENGO VYA TEHAMA SERIKALINI WAASWA KUWASHIRIKISHA WAKAGUZI WA NDANI KATIKA UJENZI WA MIFUMO YA TEHAMA


Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA Serikalini, wametakiwa kuwashirikisha Wakaguzi wa Ndani wa taasisi, katika hatua za awali za ujenzi wa mifumo na miradi ya TEHAMA ili kuhakikisha inazingatia Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao.


Wito huo umetolewa jana Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali Bw. Benjamin Magai, wakati wa kufunga mafunzo maalum kwa Wakaguzi wa Ndani wa taasisi na mashirika ya umma, yaliyofanyika mkoani Morogoro kuanzia Septemba 23 mwaka huu.

“Kila Mkuu wa Kitengo na Idara ya TEHAMA Serikalini, anapaswa kuhakikisha anawashirikisha Wakaguzi wa Ndani wa taasisi katika hatua zote za ujenzi wa mifumo na miradi ya TEHAMA kuanzia hatua za awali na hata baada ya mifumo hiyo kukamilika ili wakaguzi hao wafanye majaribio kabla ya kuanza kwa matumizi rasmi”, alisisitiza Bw. Magai.

Vilevile, Bw. Magai aliwataka Wakaguzi wa Ndani Serikalinj kuchukua tahadhari kubwa katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuhakikisha usalama wa mifumo pamoja na kuzingatia weledi ili kuzuia udukuzi katika mifumo hiyo.

Naye Mwenyekiti wa washiriki katika mafunzo hayo Bw Frank Kindimba ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ameishukuru Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) pamoja na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewajengea uwezo katika usimamizi wa miradi na mifumo ya TEHAMA Serikalini.

“Kupitia mafunzo haya, washiriki wote tumepata uelewa wa pamoja kuhusu Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao na uelewa huu utatusaidia katika kufanya kazi zetu za kikaguzi kwa usahihi zaidi”, alisema Bw. Frank.

Alibainisha kuwa, mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwa washiriki kwani wamepata elimu ya usalama wa mifumo na matumizi sahihi na salama ya mifumo ya TEHAMA.

"Tutakaporejea katika vituo vyetu vya kazi tutazingatia matumizi sahihi na salama ya mifumo ya TEHAMA kwani katika mafunzo haya hatujasoma Sheria ya Serikali Mtandao pekee bali pia tumejifunza kuhusu usalama na matumizi sahihi ya mifumo", alisema Bw. Frank.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imekuwa ikiendesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali (IAG), ili kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwenye ukaguzi wa miradi na mifumo ya TEHAMA katika taasisi zao na kuhakikisha inakuwa na tija kwa Serikali.