emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WAHAMASISHENI WADAU WENU KUTUMIA MFUMO WA e-MREJESHO KUWASILISHA KERO ZAO: e-GA


WAHAMASISHENI WADAU WENU KUTUMIA MFUMO WA e-MREJESHO KUWASILISHA KERO ZAO: e-GA


Taasisi za umma nchini, zimetakiwa kuwahimiza wadau wake kutumia mfumo wa e-Mrejesho kuwasilisha kero na maoni mbalimbali sambamba na taasisi hizo kuhakikisha zinashughulikia maoni na kero hizo kwa wakati, kupitia mfumo wa e-Mrejesho ili kuendelea kujenga imani kwa wadau wake.

Wito huo umetolewa na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Subira Kaswaga, wakati wa Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama ‘Sabasaba’ yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Subira alisema, e-GA imetengeneza mfumo wa e-Mrejesho kwa lengo la kuiwezesha Serikali kupokea malalamiko, maoni na pongezi kutoka kwa wananchi ili taasisi za umma ziweze kujitathmini juu ya utendaji kazi wake kupitia mfumo huo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mfumo huu umekuwa jukwaa na kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi wake, hivyo ni muhimu taasisi za umma zihamasishe wananchi na wadau wake wote kutumia mfumo huu kuwasilisha kero au maoni yao, lakini pia taasisi nazo zihakikishe zinashughulikia maoni hayo kwa wakati na kutoa mrejesho kwa wananchi kupitia mfumo huo”, alisema Subira.

Itakumbukwa kuwa Juni 26 mwaka huu, mfumo wa e-Mrejesho ulishinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Ubunifu katika Huduma za Umma kwa mwaka 2024 ‘UN Public Service Innovation Awards’ na kutambuliwa kuwa jukwaa muhimu la mawasiliano kati ya Serikali na wananchi ambalo pia huisaidia Serikali kufanya maamuzi ya kisera kwa wakati.

“Taasisi za umma zinaweza kujitathmini juu ya utendaji wake kupitia mfumo huu kwa kubaini maeneo ambayo yanalalamikiwa kwa wingi na wateja wake ambao ni wananchi na maeneo ambayo yanayoridhisha na hivyo kuiwezesha Serikali kufanya maamuzi ya kisera kwa wakali”, alifafanua Bi. Subira.

Aliongeza kuwa, e-GA itaendelea na ubunifu wa kutengeneza mifumo mbalimbali kwa lengo la kuzisaidia taasisi za umma kuweza kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati na urahisi zaidi kupitia TEHAMA. kadri mabadiliko ya teknolojia yanavyojitokeza.

“Tutaendelea na tafiti pamoja na bunifu mbalimbali za TEHAMA lakini pia lazima tuhakikishe hatuko nyuma kwenye teknolojia zinazochipukia (Emerging Technologyies) hivyo, tutahakikisha kuwa teknolojia hizi zinazochipukia tunazitumia vema kuhakikisha zinaleta mchango chanya kwenye Serikali”, alisema Bi. Subira.

Naye mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Andrew Munare, alieleza kufurahishwa na huduma zinazotolewa na e-GA sambamba na kujifunza namna ya kupata huduma mbalimbali za Serikali kwa haraka kupitia mfumo wa huduma za serikali kwa simu ya mkononi (m-Gov).

“Nimefurahi kupata elimu kuhusu huduma za e-GA na kufahamu uwepo wa mfumo wa kutuma malalamiko, maoni na mapendekezo (e Mrejesho), ambao unatuwezesha sisi wananchi, kutuma malalamiko na mapendekezo Serikalini kwa haraka zaidi na kufuatilia malalamiko hayo tukiwa mahali popote kupitia simu ya mkononi” alisema Bw. Munare.

Hali kadhalika Bw. Charles Paul Nazi alibainisha kuwa, wananchi wamekuwa wakihangaika juu ya namna bora ya kuwasilisha maoni na malalamiko yao hivyo, kupitia mfumo wa e-mrejesho wananchi wataweza kuwasilisha malalamiko yao na kuwasiliana moja kwa moja na taasisi husika kwa kuchagua kujulikana au kutojulikana.

Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), unasimamiwa na kuendeshwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 9 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovutiya emrejesho.gov.go.tz.