Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania, imefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), jijini Dodoma na kufanya mazungumzo na e-GA kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili.
Ziara hiyo ya Vodacom ililenga mambo muhimu matatu, ikiwemo kufahamu shughuli na jitihada mbalimbali za e-GA kwenye eneo la utafiti na ubunifu zinazoendelea kituoni hapo, kutoa uzoefu kwenye bidhaa na teknolojia ya Mawasiliano kwa vijana wabunifu waliopo kituoni hapo pamoja watumishi wa e-GA na kufanya kikao cha kujadiliana kuhusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano baina ya Vodacom na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kupitia Kituo cha eGovRIDC.
Aidha, Wawakilishi kutoka Kampuni ya Vodacom walipata fursa ya kutembelea kituo hicho, na kuona tafiti na bunifu zinazofanywa na vijana wenye fani ya TEHAMA kutoka vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi wanaofanya mafunzo kwa vitendo, mafunzo kazini na wanaojitolea katika kituo hicho.