Viongozi wa taasisi mbalimbali za umma wameeleza faida za kubadilishana taarifa kidijitali kupitia Mfumo wa pamoja wa ubadilishanaji taarifa serikalini ujulikanao kama ‘Government Enterprises Service Bus’ (GovESB).
Wakizungumza na mwandishi wetu katika nyakati tofauti, viongozi hao wameeleza kuwa, mfumo wa GoVESB umekuwa na faida nyingi ikiwemo kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kuokoa muda pamoja na gharama za uendeshaji wa taasisi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel, alisema Mahakama inabadilishana taarifa na taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Mfumo wa GoVESB umesaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Mahakama kwakuwa, tunaweza kupata taarifa kwa urahisi kutoka taasisi tulizoingia nazo makubaliano na kuweza kubadilishana taarifa kidijitali, vilevile umesaidia kuongeza ufanisi na uwazi katika kuwahudumia wananchi kwa wakati”, alisema Prof. Elisante.
Naye Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Bw. Herman Mandari, alisema kabla ya kuanza kutumia mfumo wa GovESB, chuo hicho kilikuwa kikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa taarifa kutoka taasisi mbalimbali za umma.
“Kabla ya kuanza kutumia mfumo wa GoVESB, Maafisa walilazimika kuwasilisha maombi ya kupata taarifa kwa njia ya barua kwa kutembelea taasisi husika, na hivyo kuchukua muda mrefu kupata taarifa hizo, jambo lilichongia kupunguza ufanisi katika utendaji wa kazi”, alisema Mandari.
Aliongea kuwa, changamoto nyingine waliyokabiliana nayo ni utofauti wa utaratibu wa kupata taarifa kutoka taasisi moja hadi nyingine, kwani kila taasisi ina utaratibu wake wa ndani wa kupata na kutoa taarifa na pia, baadhi ya taasisi utaratibu huo hubadilika mara kwa mara, lakini kupitia GoVESB changamoto hizo zimetatuliwa na sasa wanapata taarifa zote kwa wakati.
Kaimu Meneja wa TEHAMA Chuo cha Utumishi wa Umma Bw. Elibariki Mushi, alisema mfumo wa GovESB umewasaidia kupata taarifa sahihi, zinazoaminika na zenye ubora na viwango stahiki kwa wakati, na hivyo kuimarika kwa usalama wa upatikanaji wa taarifa.
“Taarifa hizi tunazipata sehemu moja, hili ni jambo jema na mwelekeo huu ndio ulikuwa unasisitizwa na viongozi wetu, hivyo sio tu tunabadilishana taarifa ila tutabadilishana taarifa katika viwango vinavyofanana”, alisema Mushi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE) Prof. Edda Lwoga, ametoa hamasa kwa taasisi za umma ambazo hazijajiunga na mfumo wa GovESB kujiunga na mfumo, huo kwani kutokana na mapinduzi ya sayansi na teknolojia, ubadilishanaji wa taarifa ni swala ambalo haliwezi kukwepeka katika utendaji kazi
Prof. Lwoga alisema kuwa, CBE inabadilishana taarifa na taasisi saba hivyo kwa taasisi ambazo bado hazijajiunga na mfumo wa GovESB ni vigumu kubadilishana nazo taarifa na hivyo kupunguza ufanisi katika utendaji kazi.
Aidha, Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt Adolf Rutayuga, amezishauri taasisi za umma kujiunga katika mfumo huo ili kuokoa muda wa kuwahudumia wananchi, lakini pia kupunguza gharama za kutengeneza mifumo midogo midogo ya kuunganisha na taasisi nyingine.
Mfumo wa GoVESB umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuzingatia kifungu cha 48 (2) cha Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019, kinachoitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao kuanzisha na kuendesha Mfumo unaowezesha Mifumo ya TEHAMA Serikalini kuwasiliana na kubadilishana taarifa.