Meneja wa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Dkt. Jaha Mvulla, amewata vijana watafiti na wabunifu kwenye eneo la TEHAMA kuwasilisha bunifu zao katika kituo hicho, ili kuangalia namna zinavyoweza kuisaidia Serikali katika kuwahudumia wananchi.
Dkt. Jaha amesema hayo hivi karibuni, wakati akieleza umuhimu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kushiriki katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika kitaifa jijini Tanga katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari ya Popatlal kuanzia Mei 25 hadi 31 mwaka huu.
“Maadhimisho haya yanaenda sambamba na lengo la kituo chetu cha eGOVRIDC la kuchochea ari kwa vijana wa Kitanzania kufanya utafiti na ubunifu wa TEHAMA ili kukuza na kujenga uchumi wa kidijitali”, alisema Dkt. Jaha.
Alibainisha kuwa, eGOVRIDC inafanya utafiti wa teknolojia zinazoibukia kama vile Sarafu ya Mtandaoni (Digital Currency), Block chain, Internet of Things (IOT) na Akili mnemba (Aritificial Intelligence), ili kuona ni namna gani teknolojia hizo zinaweza kutumika katika kubuni mifumo itakayoisadia Serikali katika utendaji kazi pamoja na kuwarahisishia wananchi kupata huduma.
“Nitoe rai kwa vijana wa kitanzania kuleta bunifu za TEHAMA zinazohusiana na matumizi ya teknolojia mpya, ili kuweza kuzifanyia tafiti na kuona ni namna gani zitaweza kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Serikali na kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali kwa wananchi”, alisema Dkt. Jaha.
Baadhi ya washiriki waliotembelea banda la e-GA, wameeleza kufurahishwa na huduma mbalimbali zinazotolewa na e-GA ikiwa ni pamoja na bunifu za mifumo mbalimbali ya TEHAMA na matumizi ya teknolojia mpya zinazoibuka.
Bw. Evance Sombe mmoja wa washiriki waliotembelea banda la e-GA alisema kuwa, amejifunza mengi kutoka e-GA ikiwemo utafiti na ubunifu kwenye teknolojia mpya ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence) na mifumo mingine iliyosanifiwa na kutengezwa na Mamlaka kupitia Kituo chake cha Utafiti na Ubunifu.
“Nimejifunza matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba ‘Artificial Intelligence - AI’ inayolenga kujenga mifumo ya kompyuta inayoweza kufanya kazi kwa kufanana na akili ya binadamu, ni vizuri vijana kutembelea banda la e-GA, ili kuweza kujifunza mambo yanayohusu utafiti na ubunifu lakini pia kujikita katika masomo ya sayansi kwani fursa ni kubwa kwenye sekta ya TEHAMA” alisema Bw. Sombe.
Naye Bw. Hafidh Iddi mwanafunzi wa Kidato cha nne (4) katika Shule ya Msingi Mkwakani jijini Tanga, alisema amejifunza namna ambavyo e-GA imeweza kubuni na kutengeneza mifumo mbalimbali inayotumika Serikalini na namna wananchi wanavyoitumia kupata huduma za Serikali kidijitali.
“Natumaini kuwa, mara baada ya kumaliza kidato cha sita (6) nitasomea fani ya TEHAMA ili kuweza kuisaidia Serikali kubuni mifumo itakayoongeza ufanisi katika utendaji kazi na hatimaye kutoa huduma bora na kwa wakati”, alisema Bw. Hafidh.
Kutokana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia Bw. Hafidh alitoa rai kwa wanafunzi wenzake kusoma fani ya TEHAMA, ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na kuchochea ari ya ubunifu na utafiti katika maeneo mbalimbali ya teknolojia nchini.