Serikali imetengeneza Sheria, Kanuni, Miongozo na Viwango vya utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao ili kuhakikisha kuwa, Taasisi za Umma zinatekeleza jitihada hizo katika viwango na ubora unaotakiwa.
Miongozo hiyo hutoa maelekezo kwa Taasisi za Umma juu ya taratibu sahihi zinazotakiwa kufuatwa katika utekelezaji wa juhudi mbalimbali zinazohusu matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma.
Meneja Udhibiti wa Viwango vya TEHAMA Bi. Sultana Seiff amesema, “uwepo wa miongozo hii unazisaidia Taasisi za Umma katika utekelezaji wa Serikali Mtandao na kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma zitolewazo na Serikali”.
“e-GA imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa Taasisi za Umma zinazingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao katika utendaji wa shughuli za Serikali”, ameeleza Bi. Sultan
Baadhi ya maeneo ambayo Mamlaka imekuwa ikiyafanyia ukaguzi katika Taasisi za Umma ni pamoja na uzingatiwaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, uzingatiwaji wa Viwango na Miongozo katika uhifadhi data na tathmini ya mapitio ya mifumo ya TEHAMA.
Aidha, Bi. Sultana amesema, “Mamlaka imekuwa ikifanya vikao mbalimbali vya kiufundi na Taasisi za Umma kwa lengo la kutoa msaada, ushauri na elimu juu ya uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali Mtandao”.
Vilevile, Taasisi za Umma zimekuwa zikiwasilisha nyaraka mbalimbali za TEHAMA kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao, kwa ajili ya mapitio na kupata ushauri wa kiufundi na maboresho. Hadi sasa takribani nyaraka 263 kutoka Taasisi mbalimbali za umma zimefanyiwa mapitio.
Mwisho, Bi. Sultana amezitaka Taasisi zote za Umma kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao katika viwango na ubora unaotakiwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ili kujenga mifumo yenye tija.