Ushirikiano uliopo kati ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), umechangia kukua kwa matumizi ya Serikali Mtandao katika uendeshaji wa shughuli za bandari na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Abdulatif Minhajj, hivi karibuni wakati alipofanya mahojiano maalum na mwandishi wetu kuhusu mchango wa e-GA katika mapinduzi ya kidijitali kwenye Taasisi za Umma ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, e-GA imekuwa ikishirikiana kwa karibu na TPA katika ujenzi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA, ukiwemo Mfumo wa Pamoja wa Kielekroniki wa Uondoshaji wa Shehena Maeneo ya Forodha (Tanzania Electronic Single Window System - TeSWS), ambao huratibu shughuli zote za uondoshaji wa shehena maeneo ya forodha kwa njia ya kidijiti.
“Mamlaka ya Bandari - TPA imeshirikiana na e-GA na wadau wengine katika ujenzi wa mfumo wa TeSWS, mfumo huu umesaidia wateja kuwasilisha taarifa za shehena za mizigo sehemu moja, na taarifa hizi zikafanyiwa kazi kwa haraka zaidi hivyo, kuongeza ufanisi na kupunguza msongamano wa mizigo bandarini”, alisema Minhajj.
Alifafanua kuwa, mfumo wa TeSWS unawawezesha wafanyabiashara kukamilisha maombi ya vibali na maandalizi ya malipo ya kodi za forodha kidijitali, bila kwenda kwenye taasisi mbalimbali za udhibiti wa forodha, hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Minhajj aliongeza kuwa, mfumo wa TeSWS umeleta mapinduzi makubwa katika utendaji kazi wa shughuli bandarini, hivyo kupunguza msongamano wa shehena bandarini na kuongeza uwazi hasa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali
Alibainisha kuwa, kupitia mfumo wa Single Window, mteja anaweza kuwasilisha taarifa zake kieletroniki na hatimaye kuondoa usumbufu kwa mteja kulazimika kufika au kuzunguka ofisi moja hadi nyingine kufuatilia hatua za shehena ya mzigo wake.
“Kupitia Mfumo huu watumiaji wa bandari wanaweza kuwasilisha taarifa zao na kufanyiwa kazi kwa haraka zaidi lakini pia, umepunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali” alisisitiza Minhajj.
Aidha, Minhajj alibainisha kuwa, TPA imekuwa ikishirikiana vizuri na e-GA katika utengenezaji wa miongozi ya ndani ya TEHAMA na kuhakikisha wataalamu wa ndani wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara, ili kuimarisha udhibiti na usalama wa mifumo ya taasisi hiyo.
Aidha, alitaja baadhi ya mifumo inayotumika katika utendaji kazi wa TPA ambayo ni zao la e-GA kuwa ni pamoja na Mfumo wa Barua pepe Serikalini (GMS), Mfumo wa kuomba vibali vya safari nje ya nchi (e-Vibali) na Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) ambayo imesaidia kurahisisha mawasiliano na utendaji kazi ndani na nje ya taasisi hiyo.
Katika kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya mifumo ya TEHAMA, Minhajj alisema kuwa TPA inafuata na kuzingatia Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, katika ujenzi wa mifumo na miradi mbalimbali ya TEHAMA, alisema Min hajj.
Sambamba na hayo, Minhajj aliishauri e-GA, kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa TEHAMA katika teknolojia mpya ikiwemo Akili mnemba ‘Arificial Intelligence - AI’ katika ujenzi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa TEHAMA Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Sylvan Shayo alisema, e-GA imeandaa viwango na miongozo mbalimbali ya Serikali Mtandao ambayo inatoa maelekezo na taratibu zinazotakiwa kufuatwa na taasisi za umma katika ujenzi wa miradi na mifumo ya TEHAMA, ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya TEHAMA Serikalini,.
Bw. Shayo alitoa rai kwa taasisi zote za umma kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, ili kuwa na mifumo ya TEHAMA inayoleta tija kwa Serikali na wananchi kama inavyotarajiwa.
“Taasisi zote za umma, zinapaswa kutumia kwa ukamilifu miongozo hii, ili kuleta mafanikio chanya katika utendaji kazi na utoaji wa huduma za Serikali kwa umma, na kwakufanya hivi tutakuwa tumetekeleza jitihada za Serikali Mtandao kwa ufanisi zaidi”, alisema Bw. Shayo.
Aidha, Bw Shayo aliipongeza TPA kwa ushirikiano mzuri na e-GA katika jitihada mbalimbali za ujenzi wa Serikali Mtandao na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo ili kujenga Serikali ya Kidijitali.