emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

USHIRIKIANO WA e-GA NA e-GAZ WACHOCHEA MAGEUZI YA KIDIJITALI VISIWANI ZANZIBAR


USHIRIKIANO WA e-GA NA e-GAZ WACHOCHEA MAGEUZI YA KIDIJITALI VISIWANI ZANZIBAR


Ushirikiano uliopo baina ya Wakala ya Serikali Mtandao Zanzibar (e-GAZ) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), katika ujenzi wa Serikali Mtandao umetajwa kuwa chachu ya mageuzi ya kidijitali visiwani Zanzibar.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa e-GAZ Bw. Said Seif Said, alipotoa salamu za e-GAZ hivi karibuni wakati wa hafla fupi ya kufunga Kikao Kazi cha Nne cha Serikali Mtandao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.

Alisema kuwa, Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano (MOU) kati ya e-GA na e-GAZ umeleta mageuzi makubwa ya kidijiti kwa upande wa Zanzibar, kwakuwa taasisi hizo zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu na kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya ujenzi wa Serikali Mtandao.

“Tangu tuliposaini MOU na e-GA tumepiga hatua kubwa sana, mabadiliko yamepatikana na yanaonekana, nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mha. Ndomba kwa uongozi mahiri na timu nzima ya e-GA kwa kuonesha ushirikiano nasi ili kuhakikisha na sisi Zanzibar tunafika kidijitali kwa kuhakikisha mambo mazuri yanatokea bara nasi kwetu pia Zanzibar yanatokea”, alisema Bw. Said.

Aliongeza kuwa, Zanzibar inatarajia kuanza kutumia mfumo wa e-Vibali ambapo kwa sasa e-GA inashirikiana na e-GAZ kuhakikisha mfumo huo unaweza kutumika visiwani humo kwakuwa tayari unatumika bara na umeleta mafanikio makubwa tangu ulipoanza kutumika.

“Wiki hii tulikuwa na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar na moja kati ya jambo lililoonekana zuri na kumfurahisha kiongozi huyo ni namna tunavyoshirikiana na wenzetu e-GA kuhakikisha mfumo huu wa e-Vibali unatumika pia Zanzibar, naomba niwafikishie salamu za Katibu Mkuu Kiongozi anashukuru na kuwapongeza sana e-GA, kwakuwa mmekuwa si wachoyo kwa yale mazuri mnayokuwa nayo mnahakikisha nazi Zanzibar pia tunakuwa nayo”, alisema Bw. Said.

Alisema kuwa, e-GA imekuwa ikitoa msaada wa karibu kwa e-GAZ kuhakikisha ujenzi wa Serikali Mtandao unafanikiwa kwa upande wa Zanzibar ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za serikali kwa haraka na gharama nafuu mahali walipo.

Alibainisha kuwa, makubaliano ya ushirikiano huo yamesaidia kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utekekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali Visiwani Zanzibar.

Aliyataja baadhi ya makubaliano ya ushirikiano kuwa ni pamoja na kusaidiana kitaalamu, kushauriana na kupeana mafunzo baina ya wataalamu wa taasisi hizo mbili ambapo mashirikiano haya yameweza kuonekana katika utengenezaji na uimarishaji wa mifumo mbalimbali.

Aidha, Bw. Said aliipongeza Mamlaka kwa juhudi zilizofanyika na kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa wa kuhakikisha Zanzibar inafikia mapinduzi ya uchumi wa kidijitali ikiwemo juhudi za kuhakikisha mfumo wa vibali vya kusafiri nje ya nchi (e -vibali) unatumika Zanzibar.

“Napenda kuwafikishia pongezi na salamu kutoka kwa Katibu Mkuu Zanzibar ambaye amefurahishwa sana kwa jitihada zilizofanyika za kuhakikisha mfumo wa e -vibali unatumika Zanzibar” alisisitiza Bw. Said.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mha. Benedict Ndomba, alisema kuwa e-GA itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo na e-GAZ ili kuhakikisha mapinduzi ya TEHAMA Serikalini yanaimarika katika pande zote mbili za muungano na kuwawezesha wananchi kupata huduma bora na rahisi wakati wote mahali walipo.