Meneja wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ACP. Raphael Rutaihwa amehimiza Vitengo vya TEHAMA Serikalini kufuata Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao ili kujenga mifumo bora na yenye tija.
ACP. Rutaihwa amesema hayo wakati akitoa elimu kwa umma kuhusu Sheria ya Serikali Mtandao namba 10 ya mwaka 2019 na kanuni zake.
“Ni vyema kila taasisi ya umma kuhakikisha inafuata Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao ili kuwe na mifumo yenye tija na inayowasiliana na yenye matumizi sahihi ndani ya Serikali”, amesema ACP Rutaihwa.
ACP Rutaihwa amesema kuwa Sheria hii imeainisha majukumu mbalimbali ambayo taasisi zote za umma zinatakiwa kuzingatia ilikutekeleza na kufanikisha jitihada za Serikali Mtandao.
Kupitia Sheria hii, Mamlaka imepewa majukumu mbalimbali ikiwemo kusimamia, kurekebu na kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Kanuni, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao.
Aidha, majukumu mengine ya eGA ni kuhakikisha miradi yoyote ya kiutendaji inayohusiana na TEHAMA inapotaka kuanzishwa ndani ya taasisi za umma ni lazima taasisi hizo ziwasilishe andiko la mradi. Andiko hilo lizingatie taratibu za utendaji kazi wa taasisi husika ili liweze kupitiwa na kupata ruhusa ya kuendelea na miradi/mradi huo, amesema ACP Rutaihwa.
Vilevile, Mamlaka inajukumu la kutayarisha Taratibu, Kanuni Viwango na Miongozo ambayo itatumika na kufuatwa na taasisi zote za umma katika utendaji kazi wa kilasiku ndani ya taasisi za umma.
Pia, Mamlaka inajukumu la kukagua kila taasisi ya umma na kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao unafuatwa kikamilifu na kwa taasisi ambazo hazifuati sheria hii Mamlaka ya Serikali Mtandao imepewa mamlaka ya kuziwajibisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi Benedict Benny Ndomba amesema kuwa Mamlaka inatoa elimu kwa umma kupitia vipindi vya Redio, Televisheni na kutembelea taasisi mbalimbali za umma ili kuleta uelewa wa pamoja kuhusu Sheria ya Serikali Mtandao mwaka 2019 na Kanuni zake, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao na uendeshaji na utekelezaji wa miradi ya TEHAMA Serikalini.