emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

‘TWIGA CLOUD’ MKOMBOZI WA FAILI ZAKO ZA KIDIGITI


‘TWIGA CLOUD’ MKOMBOZI WA FAILI ZAKO ZA KIDIGITI


Watu wengi hupoteza mafaili yao muhimu mara tu simu au kompyuta zao zinapoharibika au kupotea, huenda hata wewe ukawa ni miongoni mwa waathirika hao. Habari njema ni kuwa mwarobaini wa tatizo hili umepatikana, na sasa mafaili yako yatakuwa salama hata kama utapoteza simu au kompyuta yako kuharibika.

Naam! Ni kupitia mfumo wa kuhifadhi mafaili yako mkondoni wa ‘Twiga Cloud’ unaweza kutunza mafaili yako wakati wowote na kuwa na uhakika wa usalama wake hata kama kifaa chako (kompyuta, simu janja, kishwambi n.k), ulichotumia kuandaa na kuhifadhi mafaili yako kitapotea au kuharibika.

Mfumo huu una moduli tatu ‘Twiga Drive,Twiga Archive na Twiga Collabora’ ambazo zote zinamuwezesha mtumiaji kufanya kazi za kuhifadhi, kutunza na kuhariri mafaili yake kwa usalama na wepesi zaidi mtandaoni.

Kupitia moduli yake ya ‘Twiga drive’, unaweza kuhifadhi picha na nyaraka zako muhimu kama vile vyeti vya kitaaluma, hati za nyumba na mashamba, video za kumbukumbu ya matukio muhimu ulizohifadhi kwenye simu yako au ulizohifadhi katika komputa yako sawa na mifumo ya kigeni kama vile ‘Google Drive’ na ‘Drop Box’.

Licha ya kuwa na uwezo wa kutunza mafaili yako kidigiti, mfumo huu una upekee zaidi kwakuwa na moduli ya ‘Collabora’ ambayo inafanya kazi kama ‘Google docs’. Kwa kupitia moduli hii ya ‘Collabora’ iliyomo katika mfumo huu, unaweza kuandika andiko lako na ukawatumia watu wengine na mkaweza kuhariri kwa pamoja, moduli hii imesanifiwa kuwezesha wananchi ikiwemo waandishi wa tafiti, waandishi wa habari na maandiko mengine ambayo yanahitaji mapitio ya mtu zaidi ya mmoja.

Kwenye ‘Collabora’ kila kitu kimekuwa rahisi sana,unaweza ukaandika andiko lako pale na ukalituma kwa watu wengine na wote wakaweza kulifanyia kazi kwa wakati mmoja iwe kwenye kuhariri au kuongezea taarifa kwenye andiko husika.

Moduli ya tatu katika mfumo huu ni ‘Twiga Archive’, module hii inamuwezesha mtumiaji kutunza nyaraka zake kidijiti, katika moduli hii nyaraka zote zitatumwa kwa kupitia teknolojia ya Akili Mnemba na ‘Machine Learning’, kwa kutumia teknolojia hiyo, nyaraka na mafaili yote yatachakatwa na kupangwa kwa ustadi zaidi kwa kuweka lebo na mpangilio (indexing and tagging) ili kumrahishia mtumiaji asipoteze muda wakati analihitaji kulifanyia kazi.

Vilevile, moduli hii imesanifiwa na teknolojia ya ‘Optical character recognition - OCR’ ambayo inamsaidia mtumiaji kutafuta faili lake kwenye mfumo kwa kutumia neno lolote analolikumbuka lililomo kwenye andiko lake, kwa sasa moduli hii ya Twiga Archive itatumika kwa taasisi na mashirika ya umma pekee.

Mfumo huu tayari upo hewani na mwananchi yeyote anaweza kuutumia, endapo utajisajili katika mfumo huu, utapata nafasi ya GB 1 kwenye Twiga Drive ili uweze kuhifadhi mafaili yako, kwa upande wa taasisi au kampuni itapewa GB 5 za bure kwa ajili ya kutunza taarifa/nyaraka zake.

Vilevile mfumo huu umezingatia usalama, unyeti wa taarifa na unapatikana muda wote kwa mtu yeyote ambaye amejisajili.

Mfumo unapatikana kupitia simu janja au kompyuta kwa kupakua aplikesheni tumizi kwenye playstore (Android), Appstore (iOS) au Microsoft (Windows) kwa kutafuta (search) ‘Twiga Cloud’ ambako kwa sasa utapata kipengele kimoja tu cha Twiga drive.

Lakini unaweza kivinjari kwa kupitia (web browser) kwa kutumia anuani ‘https://twigacloud.tz’ kujisajili na kufurahia ubunifu huu wa kitanzania kwa kupata vipengele vya twiga drive na collabora.

Mfumo wa Twiga Cloud, umesanifiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kupitia Kituo chake cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GOVRIDC)