Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imesema kuwa itaendeleza utaratibu wa kutoa mafunzo kwa Maafisa TEHAMA wa taasisi za umma ili kuwajengea uwezo na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu Serikali Mtandao.
Kauli hiyo ilitolewa Novemba 25 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA e-GA Bw.Ricco Boma, wakati akifunga mafunzo ya siku sita kwa Wachambuzi wa Mifumo ya TEHAMA kutoka katika taasisi mbalimbali za umma, yaliyotolewa na e-GA.
"Utoaji wa Mafunzo kwa Maafisa TEHAMA ni utaratibu endelevu ndani ya Mamlaka, tunajitahidi kila mwaka tuwe na mafunzo jumuishi pamoja na mafunzo maalumu (specific) katika maeneo mbalimbali ya TEHAMA na malengo yetu ni kuzifikia taasisi zote za Umma." alisema.
Aidha, Bw.Ricco aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia elimu waliyoipata katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuboresha huduma za serikali mtandao nchini na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuridhishwa na utaratibu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, wa kutoa mafunzo mbalimbali yanayolenga kuwajengea uwezo Maafisa TEHAMA ili kuwasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao yalianza Novemba 21 mwaka huu ambapo mada mbalimbali katika maeneo ya Uchambuzi wa Mifumo ya TEHAMA, Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA, Miongozo, Viwango, Usimamizi, Ubora na Usalama wa Mifumo ya TEHAMA Serikalini zilitolewa.