Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Eng. Benedict Ndomba amesema kuwa eGA imepewa mamlaka na wajibu wa kuratibu kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na miongozo kuhusu Serikali Mtandao katika taasisi za umma.
Kwa mantiki hiyo, Mamlaka ina wajibu wa kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanakuwa bora ili kuboresha utoaji huduma kwa umma ikiwa ni pamoja na kutengeneza mifumo mbalimbali mathalani mfumo wa E-Ticket na E-Cargo wa TRC ili kuboresha utoaji huduma kwa umma kwa urahisi, gharama nafuu na haraka zaidi.
Ameongeza kuwa, eGA iliwasiliana na TRC mwaka 2018 na kukubaliana kwa pamoja kuboresha kwa kutumia TEHAMA eneo la uuzaji na ununuzi wa tiketi za abiria na mizigo. Kwa hiyo TRC kwa kushirikiana na eGA walianza kusanifu na kutengeneza mfumo kwa kutumia wataalamu wa ndani ambao ni watumishi wa umma.
Aidha, Eng. Ndomba amebainisha kuwa mfumo umefanyiwa majaribio katika vituo 71 kwa zaidi ya mwaka mmoja na sasa TRC na eGA wamejiridhisha juu ya ufanisi na ubora wa mfumo huo na sasa unazinduliwa rasmi ikiwa ni mafanikio makubwa ya Serikali ya awamu ya Tano ya Mhe. Dkt. Johun Pombe Joseph Magufuli ya kutaka makudanyo ya mapato ya serikali kufanywa kwa njia ya mtandao.
Eng. Ndomba amesema hayo mara baada ya kushuhudia hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa mfumo mpya wa Shirika la Reli Tanzania – TRC wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroni ambao umefanywa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe (Mb) ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali ya awamu ya tano la kuhakikisha kila shirika la Serikali linakukuwa na mfumo wa malipo kielektroni ili kuboresha jitihada za ukusanyaji mapato.
Hafla hiyo fupi imefanyika tarehe 4 Aprili, 2020 katika ukumbi wa mikutano uliopo Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Wajanga Kondoro, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Ndugu Focus Sahani, Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Bw. Benedict Ndomba ambaye ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA, Menejimenti ya TRC, wafanyakazi na wanahabari.
Mhe. Kamwelwe amepongeza Shirika la Reli Tanzania kwa kushirikiana na eGA kutekeleza agizo hilo la serikali na kutengeneza mfumo wa tiketi wa kielektroniki (E-Ticket) na usimamizi wa mizigo kwa njia ya mtandao (E-Cargo) ambao kwa jumla utaondoa kabisa matumizi ya tiketi za kuandika kwa mkono.
“Serikali ya awamu ya tano imekua ikielekeza TRC kuhusu umuhimu wa matumizi ya TEHAMA ili kuboresha huduma na kuongeza ufanisi hasa katika ukusanyaji wa mapato. Nimatumaini yangu kuwa kwa kutumia mfumo huu wa kielektroni, Shirika litaimarisha uendeshaji, kupunguza matumizi, kuongeza ufanisi na ukusanyaji mapato.” alisema Mhe. Kamwelwe.
Hata hivyo Mhe. Kamwelwe amesema kuwa kwa mwaka 2017/2018 kabla ya matumizi ya mfumo wa kielektroni wa tiketi, TRC ilikua ikikusanya mapato ya Shilingi 39.7 Bilioni na baada ya kuanza kwa matumizi ya mfumo huu mapato yameongezeka na kufikia kiasi cha Shilingi 44.7 Bilioni kwa mwaka 2018/2019.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TRC Prof. John Kondoro amemshukuru Waziri kwa ujio wake, pia aliongeza kuwa miongoni mwa maagizo aliyotoa Disemba mwaka 2019 ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kielektroni wa kukata tiketi ambao sasa umekamilika na umeanza kufanya kazi.
Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania umefurahishwa na shughuli nzima ya usanifishaji na utengenezaji wa mfumo ambao umefanywa na vijana mahiri ambao ni watumishi wa umma kutoka TRC na eGA na hivyo kupunguza gharama za utengenezaji mfumo ukilinganisha na gharama ambazo zingetumika kama kazi hii ingefanywa na kampuni binafsi.
Akiongea katika Uzinduzi huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania –TRC Ndugu Focus Sahani amesema mfumo huo wa kielektroni utasaidia katika ukusanyaji mapato ya shirika. Kabla ya mfumo shirika lilikuwa linakusanya mapato ya kiwango kidogo lakini tangu mfumo uanze katika kipindi cha majaribio Shirika limekusanya mapato zaidi kuliko awali.
Ameongeza kuwa mfumo una faida nyingi hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa ‘Corona’ shirika litaweza kusimamia vizuri agizo la serikali la ’level seat’ na kupunguza mikusanyiko katika maeneo ya kukata tiketi.
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mfumo wa Mawasiliano (TEHAMA) TRC Senzige Kisenge amesema “ukiwa na kifaa chochote kinachopokea mtandao wa ‘Internet’ unatembelea Tovuti TRC utapata maelekezo na utaweza kupata tiketi yako, hatua ni rafiki na rahisi hivyo tunaomba ushirikiano kutoka kwa wateja wetu”.