Utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao katika taasisi za umma, unategemea kuwepo kwa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango, Miongozo na Mikakati Madhubuti ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika taasisi hizo yanazingatiwa.
Pamoja na kuhakikisha usalama wa matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma, uwepo wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya Serikali Mtandao husaidia pia kulinda maslahi ya wananchi ambao ndio watumiaji wa huduma zitolewazo na Serikali kupitia TEHAMA.
Sheria ya Serikali Mtandao Na 10 ya mwaka 2019, inaitaka kila taasisi ya umma kutekeleza miradi ya TEHAMA kwa kuzingatia viwango vya ufundi na miongozo inayoainishwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili kuepuka urudufu wa jitihada za Serikali Mtandao.
Kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo, taasisi yoyote ya umma inayokusudia kutekeleza mradi wa TEHAMA inatakiwa kuwasilisha andiko la mradi Mamlaka ya Serikali Mtandao, kupitia Tovuti ya Huduma za TEHAMA Serikalini ijulikanayo kama ‘Government ICT Service Portal’ (GISP), andiko hilo linapaswa kuwasilishwa wakati wa hatua ya mipango ili kupata ushauri wa kitaalam na kibali kutoka Mamlaka.
Aidha, kwa miradi ya TEHAMA inayoendelea au iliyokamilika, taasisi za umma zinapaswa kuwasilisha taarifa sahihi na kamili za miradi hiyo kupitia GISP ili e-GA iweze kupitia na kufanya tathmini ya miradi hiyo na kutoa ushauri wa kitaalamu ikiwa kuna maeneo ya kuboresha.
Mamlaka hufanya ukaguzi wa miradi, mifumo na miundombinu ya TEHAMA ili kuhakikisha usalama, ufanisi pamoja na uzingatiwaji wa viwango na miongozo ya Serikali Mtandao, ili kuleta tija na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kuleta maendeleo katika taifa.
Ili kuhakikisha usalama wa mifumo, Sheria ya Serikali Mtandao inaelekeza taasisi za umma kuhifadhi mifumo yao katika mazingira yaliyothibitishwa na Serikali, e-GA inalo jukumu la kukagua mazingira yanayotumika kuhifadhi mifumo ya taasisi za umma ili kuhakikisha mazingira hayo yamethibitishwa na Serikali, lengo ni kuhakikisha usalama wa mifumo hiyo. Aidha, e-GA inaendelea kufuatilia kwa karibu ili kubaini taasisi zinazokiuka matakwa ya Sheria katika kuhifadhi mifumo yao.
Vilevile, sheria inasisitiza pale inapowezekana ujenzi wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA ifanywe kwa kutumia wataalamu wa ndani ili kuhakikisha wataalamu wa ndani wanashiriki kikamilifu katika ujenzi na usimamizi wa miradi na mifumo ya TEHAMA, na kuwezesha kutatua changamoto zinazojitokeza kwa haraka zaidi. Hata hivyo, sheria haijazuia kutumia wataalamu wa nje au sekta binafsi katika ujenzi wa miradi ya TEHAMA isipokuwa ni lazima miradi hiyo ifuate sheria na taratibu zilizowekwa sambamba na kukidhi viwango vya serikali mtandao.
Ili kuhakikisha matumizi salama ya TEHAMA serikalini, e-GA imeandaa viwango na miongozo mbalimbali ya Serikali Mtandao ambayo inatoa maelekezo na taratibu zinazotakiwa kufuatwa na taasisi za umma katika matumizi mbalimbali ya TEHAMA.
Miongozo hiyo, inaelekeza namna ya uundaji, ununuzi, usimamiaji, na utekelezaji wa jitihada za TEHAMA, jinsi ya kulinda mifumo ya TEHAMA dhidi ya maafa, majanga au uharibifu na namna ya kudhibiti athari zinazoweza kupunguza utendaji wa taasisi za umma, umuhimu wa matumizi bora, salama na sahihi ya mifumo, data na vifaa vya TEHAMA Serikalini yatakayowezesha mifumo kuungana na kubadilishana taarifa ili kufikia dira ya Serikali ya kuwa na Mifumo ya Serikali Mtandao yenye tija na ufanisi.
Taasisi zote za umma, zinapaswa kutumia kwa ukamilifu miongozo hii ili, kuleta mafanikio chanya katika utendaji na utoaji huduma za Seriakli pamoja na kuhakikisha kuwa, siri za Serikali hazivuji kwa kutumia mwanya wa TEHAMA na hatimaye kufikia azma ya kuwa na Serikali ya Kidijiti ambayo inapatikana muda wowote, mahali popote na kwa hali yeyote ya mtumiaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mha. Benedict Benny Ndomba anasema, ili TEHAMA itumike Serikalini lazima kuwe na usimamizi unaotoa mwelekeo wa kuhakikisha teknolojia ya Habari na Mawasiliano inayotumika Serikalini, inaratibiwa na kuainisha matumizi sahihi na salama katika taasisi za umma.
Ndomba anasisitiza kuwa, taasisi zote za umma, hazina budi kuzingatia kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika utendaji kazi wao ili kujenga mifumo yenye tija na kuwa, Sheria inazitaka na kuzielekeza taasisi za umma kuwasiliana na e-GA ili kuweza kushirikiana na kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanakuwa yenye tija kwa taasisi husika na serikali kwa jumla.
“Mamlaka ya Serikali Mtandao ipo kwa ajili ya kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanakuwa yenye tija na faida kwa Serikali na wananchi sio kwa ajili ya kuzibana taasisi za umma au kuzuia matumizi ya TEHAMA” Alisisitiza.
Naye, Meneja wa Huduma za Sheria e-GA, ACP Raphael Rutaihwa anasema, uwepo wa sheria ya Serikali Mtandao na kanuni zake, unasaidia kuwezesha matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi za umma, yanayopelekea kuboresha utendaji kazi na kutoa huduma bora zinazopatikana kwa urahisi na haraka, na hivyo kuwa na Serikali ya Kidigitali iliyo imara na endelevu.
ACP Rutaihwa anasema, Sheria ya Serikali Mtandao inazitaka na kuzielekeza taasisi za umma zinazohusika na ujenzi wa miundombinu ya Serikali kama vile barabara, reli na majengo kuhakikisha kuwa, zinawekewa mazingira wezeshi kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya TEHAMA kuanzia wakati wa kuandaa michoro ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
Ili kuhakikisha tunajenga serikali ya kidijitali ni vema taasisi zote za umma zikazingatia Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, kanuni zake pamoja na viwango na miongozo ya Serikali Mtandao iliyopo. Sheria ya serikali mtandao inapatikana kupitia tovuti ya mamlaka ya serikali mtandao ambayo ni www.ega.go.tz , tovuti ya Bunge ambayo ni Bunge.go.tz na online Tv ya Mamlaka e-GA online TV.