Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. George Simbachawene, amewapongeza wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanaoshiriki programu maalum ya mafunzo kwa vitendo inayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kubuni mifumo mbalimbali ya TEHAMA, inayosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini.
Mhe. Simbachawene alitoa pongezi hizo Septemba 18, wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC) jijini Dodoma, ili kufahamu tafiti na bunifu mbalimbali zinazofanywa na vijana wa kitanzania katika kituo hicho.
“Ipo baadhi ya mifumo tunajivunia hadi sasa ikiwemo e-Mrejesho, e-Board, e-Mikutano ambayo inatokana na shughuli za ubunifu na utafiti zilizofanywa na vijana wetu, kutoka katika kituo chetu hiki kwa weledi na utalaamu mkubwa, kazi ambazo hapo awali zilikuwa lazima zifanywe na wataalamu kutoka nje ya nchi,” alisema Simbachawene.
Alisema kuwa, tayari e-GA imetengeneza mifumo mbalimbali inayorahisisha utendaji kazi wa taasisi na Idara za Serikali, hivyo ni muhimu taasisi za umma zikatumia mifumo hiyo ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi zao.
Alisema kuwa, kwa sasa dunia ipo kwenye uchumi wa kidijitali ambapo TEHAMA ni nyenzo muhimu hivyo, Serikali imewekeza na kuweka kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kujenga miundombinu na mifumo inayosaidia kuboresha ufanisi wa uendeshaji wa shughuli zake lakini pia kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
“Wizara kupitia e-GA, inasimamia na kukiboresha kituo hiki ili kifanye tafiti mbalimbali hasa kwenye teknolojia mpya kama matumizi ya ‘Blockchain technologies’, Machine Learning, Artificial Intelligence na Internet of Things (IoT) ili na sisi tusibaki nyuma kama Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza” aliongeza Simbachawene.
Aidha, aliwataka wanafunzi wanaoshiriki programu maalumu ya mafunzo kwa vitendo inayoendeshwa na kituo hicho kutumia, ujuzi na uzoefu wanaoupata kujikwamua katika soko la ajira ikiwemo kujiajiri na kutengeneza ajira kwa vijana wenzao.
“Nafasi hii mliyopata ni muhimu sana kwenu nyie lakini pia kwa manufaa ya taifa letu, hivyo itumieni kujifunza na kupata ujuzi utakaosaidia kuleta maendeleo kwa taifa letu sambamba na kukuza uchumi wetu”, alisema Simbachawene.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Malamka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mha. Benedict Ndomba alisema kuwa, kupitia uwekezaji katika ubunifu, utafiti na mazoezi katika eneo la TEHAMA inawezesha nchi kushindana katika uchumi wa kidijitali kimataifa.
“Kuna mifumo mikubwa na shirikishi ambayo imetoka katika kituo hiki ikiwemo mfumo wa e-Mrejesho ambao tayari umetambuliwa na Benki ya Dunia kama mfumo bora unaotoa ushirikishaji kwa wananchi”, alifafanua Ndomba.