Meneja Mawasiliano Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Bi. Subira Kaswaga, amezitaka Taasisi za Umma nchini kuendesha vikao kidijitali kwa kutumia mfumo wa e-Mikutano ili kupunguza gharama za uendeshaji wa vikao.
Kaswaga alitoa rai hiyo jana, alipofanya mazungumzo na mwandishi wetu ofisini kwake jijini Dodoma kuhusu faida zitokanazo na mfumo wa e-Mikutano.
Alibainisha kuwa, mfumo wa e-Mikutano unawawezesha watumishi wa Taasisi za umma kufanya vikao kidijitali mahali walipo bila kulazimika kukutana mahali pamoja na hivyo kusaidia kupunguza gharama za uandaaji na uendeshaji wa vikao.
“Mfumo huu wa e-Mikutano unazisaidia taasisi za umma kupunguza gharama za uendeshaji wa vikao, kwani watumishi hawalazimiki kusafiri na kukutana mahali pamoja ili kufanya vikao na badala yake wanaweza kufanya vikao mahali walipo”, alisisitiza.
Aliongeza kuwa, mfumo wa e-Mikutano huokoa muda ambao watumishi wangeutumia kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kwa ajili ya kufanya vikao na hivyo kutumia muda huo kutekeleza majukumu yao mengine hali inayopelekea kuongeza ufanisi.
“Mfumo huu pia unasaidia kupunguza au kuondoa kabisa gharama za kulipia leseni zinazohitajika ili taasisi za umma ziweze kutumia mifumo ya uendeshaji wa vikao kidijitali iliyojengwa na makampuni binafsi”, alifafanua.
Alisema, Mamlaka ya Serikali Mtandao ilitengeneza Mfumo wa e-Mikutano, baada ya kuona uhitaji mkubwa wa matumizi ya TEHAMA kwenye eneo la kuratibu mikutano kwa watumishi wanaokuwa katika mazingira tofauti.
Mfumo wa e-Mikutano ni rahisi na rafiki kutumia kwani mtumishi yeyote wa umma mwenye barua pepe ya serikali (GMS), anaweza kuandaa kikao na kualika washiriki wengine, na pia mfumo unawezesha kuwasiliana kwa njia ya sauti na video, alifafanua.
Mfumo wa e-Mikutano umetengezwa na wataalamu wazawa kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na pia ni mfumo salama kwakuwa, umetengezwa kwa kuzingatia usalama mkubwa kwa watumiaji.