emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

‘Single Window’: Mfumo unaoleta suluhu ya changamoto za uondoshaji wa shehena Bandarini


‘Single Window’: Mfumo unaoleta suluhu ya changamoto za uondoshaji wa shehena Bandarini


Mfumo wa Kielektroni wa Pamoja wa Uondoshaji wa Shehena Bandarini na Maeneo Mengine ya Forodha (TeSWS) maarufu kama ‘Single Window’ umerahisisha usafirishaji wa shehena zinazoingia na kutoka nchini.

Mfumo huo unaruhusu uwasilishaji wa nyaraka na taarifa zinazohusu shehena kwenye Mfumo mmoja na taarifa hizo kuchakatwa na kusambazwa na Mfumo wenyewe kwenda kwa Tasisi na wadau husika.

Hayo yamebainishwa na Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba wakati wa mahojiano na mwandishi wetu ofisini kwake jijini Dodoma.

“Mfumo huu umejengwa kwa nia ya kuwarahisishia wananchi, wafanyabiashara na Tasisi za Umma zinazohusika katika utendaji wa shughuli za forodha kuweza kufanya kazi kwa pamoja, na kubadilishana taarifa kwa urahisi bila kuzunguka katika ofisi mbalimbali kupeleka nyaraka kwa ajili ya kupata leseni au vibali vya kuagiza na kutoa bidhaa bandarini au kwenye mipaka’’Alisema Mhandisi Ndomba.

Aidha, Ndomba aliongeza kuwa, dhamira ya Serikali ya kuanzisha Mfumo huo ni kuboresha zaidi mazingira ya biashara nchini kwa hadhi ya kimataifa ili kurahisisha shughuli mbalimbali za biashara hasa kwenye biashara zinazohusisha shughuli za forodha.

“Mfumo wa ‘single window’ umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA), Wizara ya Fedha na Tasisi nyingine za Umma” alisisitiza Ndomba.

Kwa upande wake Meneja wa mradi huo kutoka e-GA Bw. Godfrey Masanja alisema kuwa, utekelezaji wa mradi huo ulianza mapema mwaka 2019 ambapo kamati ya usimamizi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliridhia utekelezaji wa Mfumo huo kwa kutumia wataalamu wa ndani ikiwemo e-GA kama mmoja wa wadau na msimamizi wa masuala ya TEHAMA Serikalini.

Bw. Masanja alisema kuwa, Mfumo huo umejengwa kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza na ya pili zimekamilika na sasa wataalamu wanaendelea na awamu ya tatu ambapo tayari usanifu na mahitaji ya kiufundi yamekwishafanyika.

“Hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu tayari kampuni 877 za wakala zimekwishaanza kuutumia Mfumo huu kati ya kampuni 1,142 za wakala”, alisema Bw. Masanja. na kuongeza kuwa,

Mfumo umepokea na kuchakata kadhia (customs declarations) 459,671, kati ya hizo zilizokamilika na kuwezesha shehena kulipiwa kodi na kutoka bandarini na maeneo mengine ya forodha ni 438,126 na kadhia zilizosalia zipo kwenye Tasisi na wadau wengine katika hatua ya ugomboaji.

Aidha, Bw. Masanja alieleza kuwa, Mfumo wa TeSWS umeunganishwa na unabadilishana taarifa na Mifumo mingine, ikiwa ni pamoja na Mfumo wa kuondosha Shehena katika Maeneo ya Forodha (TANCIS) wa TRA pamoja na Mifumo ya Tasisi za Udhibiti ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC).

Ujenzi wa Mfumo wa “single window” ni moja ya jitihada za Mamlaka ya Serikali Mtandao za kukuza matumizi ya TEHAMA Serikalini kwa kushirikiana na Tasisi mbalimbali za Umma katika kuijenga Serikali ya Kidijitali ili kuhakikisha kuwa huduma kwa Umma, wafanyabiashara pamoja na wageni zinapatikana kwa urahisi, haraka na gharama nafuu.