emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

SIMBACHAWENE: TUTAHAKIKISHA MATUMIZI YA TEHAMA SERIKALINI YANAZIDI KUIMARIKA


SIMBACHAWENE: TUTAHAKIKISHA MATUMIZI YA TEHAMA SERIKALINI YANAZIDI KUIMARIKA


Serikali imeahidi kuendelea kusimamia na kuhakikisha matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma yanaimarika zaidi, ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali kwa wananchi kidijitali.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. George Simbachawene, wakati akifungua Kikao Kazi cha 4 cha Serikali Mtandao kilichofanyika kwa siku tatu kuanzia Februari 06 hadi 08, mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2021/22 - 2025/26), kwa pamoja zinatambua nafasi ya TEHAMA katika kufikia malengo ya taifa, na hivyo kusisitiza juu ya matumizi sahihi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali na utoaji wa huduma kwa umma”, alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016, inasisitiza juu ya Serikali kutumia fursa zitokanazo na TEHAMA pamoja na matumizi sahihi na yenye tija ya Mifumo ya TEHAMA, katika kuboresha utendaji kazi wa taasisi, unaosaidia kutatua changamoto za kiutendaji, kudhibiti mapato ya Serikali, kujenga na kuboresha uwezo, pamoja na kuimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau wa Serikali.

Alibainisha kuwa, Wizara yake imepewa dhamana ya kuratibu na kusimamia matumizi ya TEHAMA Serikalini ili kuhakikisha dhamira ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. ya kuijenga Serikali Mtandao inatimia, kwa kuhakikisha huduma zote za Serikali zinapatikana kidijitali na kuwawezesha wananchi kupata huduma hizo kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu mahali walipo.

“Ili kufikia malengo ya kuwa na Serikali Mtandao, Rais ameelekeza kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika Taasisi za Umma inawasiliana na kubadilishana taarifa kidijitali ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Wizara imetekeleza agizo hili kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kutengeneza Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini ujulikanao kama GoVESB”, alisema Simbachawene na kuipongeza e-GA kwa kutekeleza agizo la Rais.

Alisisitiza kuwa, taasisi zote za umma zinapaswa kujiunga kwenye mfumo wa GoVESB ili kubadilishana taarifa kidijitali, kama ambavyo Mhe. Rais amekuwa akisisitiza Taasisi za umma zibadilishane taarifa kidijitali.

“Kama isemavyo kauli mbiu ya kikao kazi hiki “Uzingatiaji wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Ubadilishanaji Salama wa Taarifa”, ni muhimu kuwa na mifumo pamoja na miundombinu ya TEHAMA inayozingatia Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao ili tuweze kubadilishana taarifa kidijitali na kwa usalama”, alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi, alisema kwamba katika kuhakikisha TEHAMA inaimarika Serikalini, Wizara itaendelea kuboresha miundo ya kiutumishi pamoja na stahiki kwa wataalamu wa TEHAMA ili kuhakikisha wanatumia taaluma zao ipasavyo kuleta matokeo chanya kwa taifa.

“Wizara inatambua kuwa, mafanikio ya Serikali Mtandao ni jumuishi kwa kada zote, niwahakikishie kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kada zote ili kufanikisha ujenzi wa Serikali ya Kidijitali”, alisema Bw.Mkomi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mha. Benedict Ndomba alisema kuwa, katika utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA Serikalini inawasiliana na kubadilishana taarifa ambapo, hadi kufikia Januari mwaka huu Taasisi za Umma 109 zimeunganishwa katika mfumo wa GovESB na mifumo 117 imesajiliwa.

Kikao hicho cha siku tatu, kiliwakutanisha takriban wadau zaidi ya 1000 kutoka katika Wizara, Wakala, Idara, Taasisi na Mashirika ya Umma na kujadiliana kuhusu utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, kuainisha changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo.