Serikali imesema imejipanga kuboresha mifumo ya TEHAMA Serikalini ili kuhakikisha uwajibikaji na utendaji kazi wa Serikali unaimarika na kuwa haitosita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayetaka kuchezea mifumo hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama wakati akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 16, 2022 Jijini Dodoma.
Waziri huyo amesema kuwa Wizara yake kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imetengeneza mifumo mbalimbali ya kiutendaji inayomrahisishia mwananchi kupata huduma za Serikali kwa urahisi na mahali popote na wamejipanga kuhakikisha hatokei mtu yeyote ndani wala nje ya nchi atakayechezea mifumo hiyo.
‘’Kupitia Sheria, Kanuni na Taratibu za Serikali Mtandao tulizonazo hatutaona aibu kumchukulia hatua mtu yeyote atakayetaka kuchezea mifumo hii ya Serikali ambayo inataka kuleta tija kwa watanzania na kutengeneza uchumi endelevu kwenye Taifa hili’’ amesema Waziri Mhagama.
Aidha katika kutekeleza agizo la Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha Mifumo ya TEHAMA ndani ya Serikali inawasiliana na kubadilishana taarifa ili kupunguza mianya ya rushwa na gharama za utoaji huduma, Waziri Mhagama amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imekamilisha kutengeneza Mfumo wa Government Enterprise Service Bus (GovESB) mfumo ambao unaiwezesha Mifumo mbalimbali ya Serikali kubadilishana taarifa.
Aidha, Waziri Mhagama ameongeza kuwa kupitia Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanikiwa kuanza na kujenga Mfumo mbalimbali ikiwemo mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma Public EmployeesManagement Information System (PEPMIS) ili kuondokana na changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS, ambao haukuakisi hali halisi ya utendaji kazi wa watumishi hali iliyoleta hisia za kupendeleana, kuoneana na kutokutumika kwa matokeo ya utendajikazi katika kufanya maamuzi ya kiutumishi.
Vilevile, amesema Mfumo huo mpya wa PEPMIS utapunguza na kuondoa matumizi ya makaratasi, utaongeza uwazi katika usimamizi wa watumishi na kuondoa upendeleo na uonevu katika upimaji wa utendaji kazi kwa watumishi.
Pia, Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi ujulikanao kama Public Institutions Performance Management Information System (PIPMIS) ambao ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi ya Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika itayatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo makubaliano hayo yatakuwa kati ya viongozi wakuu wa Taasisi na Viongozi wao wanaowasimamia katika masuala ya kisera na utendaji wa kila siku.
‘’Utekelezaji wa Mfumo wa huu wa PIPMIS utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sera, mikakati na vipaumbele vya taasisi, sekta na Taifa kwa ujumla; kuimarisha utamaduni unaojali matokeo; na kuleta matumizi bora ya rasilimali za umma. Manufaa haya yatatokana na kuwepo kwa vigezo na viashiria vya kupima utendaji wa taasisi katika maeneo hayo, kulinganisha na kushindanisha utendaji wa taasisi na kutoa tuzo za utendaji mzuri kila mwaka’’ Waziri Mhagama.
Sanjari na hayo, katika kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Serikali Mtandao na kujenga mifumo ya TEHAMA, Waziri huyo ameitaja mifumo mingine iliyojengwa ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuwa ni pamoja na Mfumo wa Sema na Waziri wa UTUMISHI, Mfumo wa e-Mrejesho ambao unapatikana kwa anuani ya e-mrejesho.gov.go.tz. , Mfumo Maalum wa Tathmini ya Hali ya Rasilimaliwatu (Human Resource Management Assessment System) ,Mfumo wa Huduma Mtandao kwa Watumishi (Watumishi Portal) ambao ni sehemu ya Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) pamoja na Mfumo wa Kupima Mienendo na Tabia za Wanaoomba Nafasi za Ajira Serikalini (Psychometric Test).