emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

SERIKALI YAJIPANGA KUPUNGUZA PENGO LA KIDIJITI NCHINI


SERIKALI YAJIPANGA KUPUNGUZA PENGO LA KIDIJITI NCHINI


Serikali imesema kuwa, itaendelea kupunguza pengo la kidijiti lililopo kati ya mijini na vijijini ili kuhakikisha mapinduzi ya kidijitali yanaleta maendeleo chanya na usawa katika maeneo yote sambamba na kuboresha hali ya kiuchumi kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi, wakati akifungua warsha ya mafunzo na mashauriano ya siku mbili kuhusu usimamizi wa huduma za umma na mfumo wa utawala wa data ‘Capacity Development and Consultation Workshop on Public Service Management and Data Governance Framework’ iliyofanyika Agosti 21, jijini Dodoma.

Alisema kuwa, Serikali imeendelea kuwekeza katika teknolojia ikiwemo kuboresha miundombinu ya teknolojia, ujenzi wa mifumo mbalimbali sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA Serikalini, katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia.

“Serikali kupitia e-GA, imeanzisha mifumo inayowezesha wananchi kupata huduma za Serikali kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na mfumo unaowezesha wananchi kutuma, kupokea na kushughulikia malalamiko, Mapendekezo, Maulizo na Pongezi ‘e-Mrejesho’, Mfumo wa Malipo Serikalini ‘GePG’ pamoja na Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia Simu za Mkononi ‘ MGoV’”, alisema Bw. Xavier.

Alifafanua kuwa, katika kupunguza pengo la kidijiti nchini, matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika utoaji wa huduma kwa umma, ni moja ya mkakati unaofanywa na Serikali ili kuhakikisha wananchi wote waishio mijini na vijijini, wanapata huduma kwa urahisi na haraka mahali walipo bila ya upendeleo.

Alibainisha kuwa, juhudi hizi zinazofanywa na e-GA zinalenga kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia ili kuboresha utoaji wa huduma kwa umma, kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali katika maeneo yote pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Bw. Xavier alisisitiza kuwa, serikali imedhamiria kuharakisha matumizi ya teknolojia yanazidi kuimarika kwa kuweka mazingira mazuri ya uwezeshaji ya kisera, kisheria pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA katika teknolojia zinazoibukia ili zitumike vizuri na kuleta tija kwa Taifa.

“Tunaendelea kuimairisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa TEHAMA kama ambavyo leo tunashuhudia ushirikiano huu kati ya yetu sisi Serikali na Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (UN DESA), hii inaashiria dhamira tuliyonayo ya kuhakikisha tunafikia malengo ya ujenzi wa Serikali ya kidijiti kwa ushirikiano wa pamoja na taasisi zisizo za kiserikali”, alisema Bw. Xavier.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi. Benedict Ndomba alisema kuwa, e-GA itaendelea kusimamia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, ili kuhakikisha mifumo na miradi ya TEHAMA Serikalini inaleta tija iliyokusudiwa.

Alibainisha kuwa, warsha ya usimamizi wa huduma za umma na mfumo wa utawala wa data ‘Capacity Development and Consultation Workshop on Public Service Management and Data Governance Framework’ ni muhimu kwa viongozi na Maafisa TEHAMA Serikalini, kwani inawapa elimu juu ya namna ya kusimamia eneo hilo kwa ufanisi zaidi.

Naye Bi. Shabnam Mallick, Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Makazi Umoja wa Mataifa alisema, matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi Serikalini ni kichocheo kikubwa cha kufikia dhima ya maendeleo endelevu.

Alibainisha kuwa, matumizi ya teknolojia zinazoibukia yatasaidia Serikali kuongeza ufanisi, uwazi na ushirikishwaji katika huduma na hatimaye kuchangia katika maendeleo endelevu ya nchi.

Bi. Mallick amesema, pengo la kidijiti lililopo kati ya mijini na vijijini linazuia uwezo wa kutumia kikamilifu faida zipatikanazo na matumizi ya mifumo ya kidijitali na hata kufikia

“ Ili kukabiliana na changamoto hii ya pengo la kidijiti, mbinu za kina zinahitajika ikiwa ni pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika taarifa, matumizi ya teknolojia mpya zinazoibuka ikiwemo Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) na pia Serikali inapaswa kuweka kipaumbele katika ujuzi wa matumizi ya teknolojia” alisema Bi. Mallick.

Warsha ya Usimamizi wa Huduma za Umma na Mfumo wa Utawala wa Data ‘Capacity Development and Consultation Workshop on Public Service Management and Data Governance Framework’ iliandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (UN DESA),