Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa bunifu mbalimbali za Mifumo ya TEHAMA inayorahisisha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Rosemary alitoa pongezi hizo hivi karibuni, wakati alipotembelea banda la maonesho la e-GA katika maadhimisho ya wiki ya kitaifa ya ubunifu na MAKISATU, yaliyofanyika April 24 hadi 28 mwaka huu katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma.
"Taasisi yetu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kweli mmekuwa mkifanya kazi nzuri, mmetutoa katika yale mambo ya kizamani ya kurundikana kwa makaratasi ofisini mmetuletea Mifumo ambayo sasahivi hata kama nisipokuwa ofisini bado naweza kujibu barua, mimi nawapongeza sana" alisema Rosemary.
Katika Maonesho hayo, e-GA kupitia kituo chake cha Utafiti na Ubunifu wa Maendeleo ya Serikali Mtandao (eGovRIDC) imeonesha teknolojia na bunifu mbalimbali zilizobuniwa na vijana wa kitanzania ambazo zimelenga kuimarisha na kukuza jitihada za Serikali Mtandao.
Baadhi ya Mifumo iliyooneshwa ni pamoja na; Mfumo wa kuratibu shughuli za kimawasiliano kwa kupiga simu kwa Taasisi mbalimbali za Umma (Intergrated CallCenter System & CRM), Ubunifu unaotumia Teknolojia ya akili bandia (Artificial Intelligence) kusaidia Mamlaka ya Serikali Mtandao kujibu maswali ya mara kwa mara kuhusiana na utendaji kazi wa Mamlaka (ChatAI);
Ubunifu wa ndani wa mtandao wa ‘Blockchain’ unaohimiza matumizi ya mtandao wa ‘Blockchain’ kutengenza mifumo mbalimbali (Alphachain Blockchain Network), ubunifu wa mtandao unaotokana na Teknolojia ya ‘Blockchain’ yenye malengo ya kuongeza ulinzi kwenye matumizi na utumaji wa nyaraka mbalimbali (Sec doc);
Mingine ni Mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, maulizo na pongezi kwenda kwa Taasisi mbalimbali za Umma (eMrejesho), Mfumo wa kuratibu vikao vya bodi na kamati zake, Menejimenti na kamati zake pamoja na Madiwani (eBoard);
Ubunifu wa mtandao wa kijamii ulio salama ulioundwa kwa lengo la kufanya mawasiliano kupitia simu za mkononi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi, simu za sauti pamoja na simu za video (Oxygen) na ubunifu wa Teknolojia unaofanania na ‘TeamView’ na ‘Anydesk’ unaoruhusu kubadilishana skrini za kompyuta kwa watu walio kwenye maeneo tofauti ya kijografia ambao pia unaruhusu utumaji na upokeaji wa majalada mbalimbali kwa njia ya kielectroni (RSS).
Aidha, wananchi waliotembelea katika banda la e-GA licha ya kufurahishwa na bunifu za mifumo hiyo, pia waliishauri Mamlaka kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mifumo hiyo na namna inavyotumika.
Maonesho ya wiki ya Ubunifu Tanzania mwaka 2023 yameandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikisha na Taasisi za Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo, Vyuo vya Ufundi, Mashirika na Taasisi za Umma, Mashirika na Taasisi binafsi za Teknolojia, Wizara mbalimbali na wabunifu walioendeleza katika programu ya MAKISATU.