Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewata watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kufanya kazi kwa kibidii na kuongeza ubunifu katika eneo la TEHAMA, ili kuibua mifumo itakayoweza kutatua matatizo ya watanzania.
Ridhiwani alisema hayo hivi karibuni, wakati wa kikao kazi cha watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao kilichofanyika katika ofisi za Mamlaka zilizopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Kwakuwa dunia inaendeshwa kidijitali, matumizi ya teknolojia hatuwezi kuyakwepa hivyo, watumishi wa Mamlaka hamna budi kuongeza ubunifu katika eneo la TEHAMA kwa kutengeneza mifumo inayotatua matatizo tuliyonayo, alisema.
“Tunategemea kupitia e-GA mambo yote yataenda kidijitali, mmefanya kazi kubwa sana tunaiona kwakuwa huduma nyingi za serikali kwa sasa zinapatika kidijitali lakini ni lazima muendeleze ubunifu kwakuhakikisha mnaibua mifumo mbalimbali inayotatua matatizo tuliyonayo”, alisisitiza.
Aliongeza kuwa, teknolojia hukua na kubadilika kila siku, hivyo ni lazima watumishi wa e-GA wakajiendeleza kwa kupata mafunzo ya mara kwa mara ya muda mfupi na mrefu, ndani na nje ya nchi ili kuendana na mabadiliko hayo.
“Wizara ipo tayari muda wowote kutoa msaada pindi mtakapohitaji, ni lazima mjifunze kutoka kwa wenzetu waliotuzidi kwa upande wa teknolojia, hivyo uongozi wa e-GA muweke utaratibu wa kuwawezesha watumishi wenu kupata mafunzo ndani na nje ya nchi”, alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Eng. Benedict Ndomba, aliahidi kutekeleza maagizo ya Naibu Waziri ikiwa ni Pamoja na kuandaa utaratibu wa kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kupata mafunzo mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Kikao kazi hicho kiliongozwa na Mhe. George Simbachawene Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Naibu Waziri Mhe. Ridhiwani Kikwete pamoja na Katibu Mkuu Bw. Juma Mkomi.