Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb), amezitaka Taasisi za Umma zenye kiwango kidogo cha utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao, kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA ili kuleta tija katika utendaji kazi wao.
Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo Februari 13 mwaka huu, wakati akifunga Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao kilichofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa AICC jijini Arusha na kuhudhuriwa na washiriki takriban 1500 kutoka katika taasisi za umma na binafsi.
Alisema kuwa, Serikali imedhamiria kuimarisha na kupanua wigo wa matumizi TEHAMA, ili kwenda sambamba na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwa shughuli nyingi duniani zikiwemo za kiuchumi kwa sasa zinafanyika kwa kutumia TEHAMA.
Waziri Simbachawene alibainisha kwamba, Serikali imeweka kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA hususan katika masuala ya utafiti na ubunifu, ili kuwa na mifumo ya TEHAMA itakayotatua changamoto zilizopo nchini kwa ufanisi zaidi kulingana na mazingira husika.
‘‘Pamoja na hayo tumedhamiria kuimarisha usalama wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini pamoja na kuongeza idadi ya watumiaji wa intaneti, ili kuhakikisha wananchi wanazifikia huduma za Serikali kidijitali mahali walipo,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, kutokana na kasi ya ongezeko la matumizi ya simu za mkononi, Wizara kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imejipanga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma nyingi za serikali, zinapatikana kupitia simu za mkononi.
‘‘Tunajivunia kuona idadi ya watumiaji wa simu za mkononi pamoja na intaneti inaongezeka mwaka hadi mwaka, ongezeko hili linatupa chachu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi ili ziwafikie wananchi wengi zaidi na kwa urahisi,” alisisitiza Mhe.Simbachawene
Aidha, Mhe.Simbachawene alizielekeza taasisi za umma kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha zinatumia fursa ya ongezeko hili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kidijitali kupitia simu za mkononi.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu Bw. Mulula Mahendeka alisema, vikao kazi vya Serikali Mtandao vinavyofanyika kila mwaka, vimekuwa na manufaa makubwa katika kukuza na kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao, kupitia mawazo mbalimbali yanayotolewa na washiriki wa vikao hivyo.
Alibainisha kuwa, katika kila kikao kumekuwa na maazimio yanayowekwa na washiriki yanayolenga kuboresha ukuaji wa Serikali Mtandao nchini, na kuahidi kusimamia utekelezaji wa maazimio ya Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao.
‘‘Niwaahidi washiriki wote kuwa Wizara itasimamia utekelezaji wa maazimio yote mliyoyaweka katika katika Kikao Kazi hiki ikiwa maazimio hayo yanaihusu Wizara yenyewe, e-GA au taasisi nyingine ya umma,” alisisitiza Bw. Mahendeka.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi. Benedict Ndomba, aliwashukuru washiriki wa kikao hicho na kuwakumbusha kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika uanzishwaji na uendeshaji wa miradi mbalimbali ya TEHAMA.