Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuendelea kufanya utafiti na ubunifu wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuibua Mifumo itakayosaidia kuimarisha sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji ili kuleta maendeleo kwa taifa.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo wakati akifungua kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya TEHAMA katika Taasisi za Umma, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) haina budi kufanya tafiti zitakazowezesha ubunifu wa Mifumo itakayoboresha utendaji kazi katika Taasisi za Umma na hivyo kuchochea utoaji wa huduma bora kwa wananchi”, alisisitiza Mhe. Ndejembi.
Aidha, Mhe. Ndejembi alisema kuwa, Serikali ya awamu ya sita imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA hususani katika masuala ya utafiti na ubunifu kwenye eneo la TEHAMA ili kuimairisha uchumi wa kidigitali katika sekta ya viwanda na biashara.
“Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Umma na Utawala Bora, itaendelea kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria pamoja na kuijengea uwezo Mamlaka ya Serikali Mtandao ili iweze kufikia malengo iliyojiwekea”, alisisitiza Mhe. Ndejembi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro, alisema kuwa utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni moja ya maeneo muhimu ya maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanywa katika Utumishi wa Umma ambayo yamesaidia kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa Umma.
Dkt. Ndumbaro alisema kuwa, Serikali imeweka mazingira mazuri ya kisera, kisheria, na kiusimamizi ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya TEHAMA katika Taasisi za Umma na yanayoleta tija na ufanisi unaoboresha utendaji kazi wa Taasisi hizo na kuwaondolea wananchi kero mbalimbali.
“Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaunga mkono juhudi za Serikali za kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma za Serikali kidijiti ili kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma” alisema Dkt. Ndumbaro.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Eng. Benedict Ndomba alisema, katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, e-GA imefanikiwa kuyatimizia malengo mbalimbali iliyojipangia kwa ufanisi mkubwa kutokana na uzingatiaji wa Misingi Mikuu sita (6) inayoongoza utendaji kazi ndani ya Mamlaka, ambayo ni weledi, ubunifu, ushirikiano, kuthamini wateja, uadilifu, na kufanya kazi kwa pamoja.
Eng. Ndomba alisema kuwa, ushirikiano na utendaji kazi mzuri na wadau wa Serikali Mtandao umeisadia Mamlaka kufika malengo yake ya kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za umma yanakuwa na tija na ufanisi ili kurahisiaha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa urahisi na haraka pamoja na kuhoresha huduma hizo.
“Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma imefanikiwa kusanifu, kujenga na kusimamia uendeshaji wa Mifumo na Miundombinu mbalimbali ya Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma ili kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma mpya za Serikali Mtandao kwa Umma”, alisema Eng. Ndomba.
Aidha, Ndomba alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Mamlaka katika uendeshaji na usimamizi wa Mifumo kuwa ni pamoja na; baadhi ya Taasisi kuwa na Mifumo isiyobadilishana taarifa, Mifumo isiyowasiliana na Mifumo mingine pamoja na upungufu wa nyenzo muhimu za kukabiliana na matishio ya usalama wa mtandaoni yanayoongezeka kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.
Kikao Kazi cha 3 cha Serikali Mtandao, kilifanyika Februari 8 hadi 10 mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) na kuwakutanisha wadau 1624 wa Serikali Mtandao kutoka katika Mashirika na Taasisi za Umma, kwa lengo la kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza Serikali Mtandao nchini wakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Mifumo Jumuishi ya TEHAMA kwa Utoaji wa Huduma Bora kwa Umma”.
......................................................MWISHO.....................................................