emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

e-GA YAPONGEZWA UJENZI WA MIFUMO YA KIELEKTRONIKI SERIKALINI


e-GA YAPONGEZWA UJENZI WA MIFUMO YA KIELEKTRONIKI SERIKALINI


NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Clement Sangu (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kutengeneza mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa fedha za Serikali ambayo imesaidia kuzuia upotevu wa fedha za umma.

Mhe. Sangu amesema hayo Septemba 05 mwaka huu, wakati alipotembelea Makao Makuu ya Ofisi za e-GA zilizopo Mtumba jijini Dodoma, na kufanya mazungumzo na watumishi wa e-GA, ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika ofisi hiyo tangu kuteuliwa kwake.

Alisema kuwa, e-GA imefanya kazi nzuri ya kusanifu na kutengeneza mifumo inayoisaidia Serikali katika ukusanyaji wa maduhuli na kuchangia kudhibiti mianya ya rushwa na upotevu wa fedha za umma.

“Kupitia mifumo mliyotengeneza e-GA, kwa sasa sisi kama Serikali tunaweza kukusanya fedha vizuri kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwani, kupitia mifumo ya kielektroniki fedha zote huenda Serikalini, hivyo jukumu linalobaki ni sisi viongozi na watumishi wa umma kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa weledi”, alisema Mhe. Sangu.

Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha mifumo inayotengezwa inakuwa thabiti na kuleta matokeo chanya kwa serikali, ni lazima watumishi wa e-GA wanaotengeneza mifumo hiyo waendelee kuwa wazalendo na waadilifu kwa kufanya kazi kwa maslahi mapana ya Taifa na kutoa ushirikiano unaohitajika kwa Serikali.

“Vilevile, niwapongeze e-GA kwa kusanifu na kutengeneza mifumo ya TEHAMA inayotumika katika taasisi mbalimbali za umma ambapo, hapo awali mifumo hiyo ilikuwa inatengenezwa na wakandarasi jambo ambalo limesaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali”, alisisitiza Mhe. Sangu.

Aliitaja baadhi ya mifumo iliyotengenezwa na e-GA na inatumika katika taasisi mbalimbali za umma kuwa ni pamoja na Mfumo wa Barua Pepe za Serikali (GMS), Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), na Mfumo wa Malipo Serikalini (GEPG), na kuitaka e-GA kuendelea kuisimamia vyema mifumo hiyo na kuimarisha usalama wake ili iendelee kufanya kazi vyema zaidi.

Sambamba na hilo, Mhe. Sangu aliitaka e-GA kufanya mapitio na tathmini ya utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma, ili kuhakikisha Taasisi za Umma zinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Serikali Mtandao.

“Najua mnafanya kazi vizuri lakini, nawakumbusha kuwa mnapaswa kuendelea kufanya tathmini ya miradi mbalimbali ya TEHAMA Serikalini ili kuhakikisha taasisi zote za umma zinazingatia Sheria ya Serikali Mtandao, Viwango na Miongozo ili miradi hiyo ilete tija kwa Serikali”, alisisitiza Mhe. Sangu.

Alifafanua kuwa, ikiwa Taasisi za Umma zitazingatia Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika hatua za uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya TEHAMA , itasaidia kuondoa urudufu wa mifumo na kuokoa fedha za Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, alimshukuru Mhe. Sangu kwa ziara hiyo na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyotoa ikiwa ni pamoja na kuimarisha uadilifu na uzalendo kwa watumishi wa e-GA.