emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mtumishi Mahiri e-GA 2023: MWANAASHA SEMBOKO


Mtumishi Mahiri e-GA 2023: MWANAASHA SEMBOKO


Afisa TEHMA Mwandamizi kutoka Idara ya Usimamizi wa Huduma za TEHAMA Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Mwanaasha Semboko ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha kumchagua Mtumishi Mahiri wa Mamlaka kwa mwaka 2023.

Hayo yalibainishwa na Meneja wa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Bw. Erick Kalembo wakati wa mahojiano na mwandishi wetu jijini Dar Es Salaam kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) 2023.

“Mchakato huu wa kupata mtumishi mahiri ulianza kwa kufanya uchaguzi wa mfanyakazi bora ndani ya idara pamja na vitengo, ambao ulikua wa wazi na huru kwa watumishi wenyewe kufanya tathmini kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na kisha kupiga kura”, alisema Bw. Kalembo.

Baada ya kupata mtumishi bora kwenye kila idara na vitengo Menejimenti ya Mamlaka ilifanya kikao na kupokea orodha ya majina ya watumishi waliochaguliwa na kisha kupiga kura kwa ajili ya kuwapata watumishi watatu bora wa Mamlaka, ambapo Bi. Mwanaasha aliibuka mshindi baada ya kupata kura nyingi akifuatiwa na Bw. Masuka Manyasi na Bi. Dhulfa Abdallah aliyeshika nafasi ya tatu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) kutoka e-GA Bw. Asraji Juma alisema mojawapo la takwa la kisheria kwenye Chama cha Wafanyakazi ni lazima kila taasisi ichague watumishi bora katika idara na vitengo ambao kati yao atapatikana mtumishi mahiri wa taasisi baada ya watumishi hao kushindanishwa na kuipongeza e-GA kwa kuzingatia sharia hiyo.

Naye Bi. Mwanaasha alishukuru Menejimenti ya e-GA kwa kumchagua kwakuwa inaonesha kuthamini mchango na juhudi zake katika taasisi jambo linalompa moyo kuendelea kufanya kazi vizuri Zaidi kwa kuzingatia sharia na taratibu za utumishi wa umma.

“Ninaishukuru sana Manejimenti ya e-GA kwa kuniona, kuniamini na kunichagua kuwa Mtumishi Mahiri kwa mwaka 2023, nimefarijika sana kwani sikutegemea na sikujua kama watu wanaona kazi kubwa ninayoifanya na kuithamini pia ninahaidi sitowaangusha nitafanya kazi kwa moyo wa kujituma, bidi na weledi kubwa zaidi”, alisema Bi. Mwanaasha.

Vilevile, Mwanaasha aliwashukuru watumishi wote wa Mamlaka hususan timu yake ya kukusanya madeni, kwa kukubali mawazo na ushauri mbalimbali aliokua akiutoa pamoja na ushirikiano wao katika kutimiza majukumu yao ya kila siku jambo iliyopelekea yeye kuibuka kuwa mtumishi mahiri.

Pia, amewashauri watumishi wote kufanya kazi kwa kujituma, kujitoa na kujiamini na sikuzote wakumbuke kuwa hakuna kazi ngumu kitu cha muhimu ni kila mtumishi kupambana na kuhakikisha anatatua changamoto zilizopo ili kufikia malengo ya taasisi.

Bi. Mwanaasha pamoja na watumishi wote waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora mwaka 2023 walipewa zawadi za fedha tasilimu ikiwa ni motisha kwa watumishi wengine kuendelea kufanya kazi vizuri Zaidi na kwa weledi.