emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MIAKA 3 YA RAIS DKT. SAMIA: SERIKALI MTANDAO YAZIDI KUIMARIKA


MIAKA 3 YA RAIS DKT. SAMIA: SERIKALI MTANDAO YAZIDI KUIMARIKA


Ilianza siku na hatimaye miaka mitatu sasa imetimia tangu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuingia madarakani.

Ilikua Ijumaa ya Machi 19 mwaka 2021, siku ambayo historia iliwekwa kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuapishwa rasmi na Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuanza kuongoza rasmi Serikali ya Awamu ya Sita.

Siku hii ilikuwa ya kihistoria kwa Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwakuwa na mwanamke wa kwanza kuwa Rais, na jemedari mahiri katika anaijenga Tanzania mpya ya Kididjitali, kuweka vipaumbele mbalimbali vya kitaifa kwa maendeleo ya nchi na kusisitiza uzalendo, kuleta umoja, mshikamano, kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo pamoja na kufanya kazi kwa bidii.

Katika kuhakikisha dhamiria ya ujenzi wa Serikali ya Kidijitali, moja ya vipaumbele alivyoviweka Mhe. Rais, Dkt Samia ni kuimarisha matumizi ya TEHAMA Serikalini kwa kuhakikisha TEHAMA inatumika kwenye utendaji kazi ili kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za Serikali kwa wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict B. Ndomba, anasema kuwa kumekuwa na mafanikio chanya katika matumizi ya TEHAMA Serikalini, ambayo yamechochewa na utayari wa Serikali ya awamu ya sita.

Anabainisha kuwa, uwepo wa dira mahususi kuhusu Sera ya TEHAMA, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao pamoja na mikakati madhubuti na utekelezaji wa kizalendo unaosimamiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), umechochea kuimarika zaidi kwa matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma.

“Katika miaka mitatu ya Mhe. Dkt. Samia tunashuhudia kuimarika kwa miundombinu bora na shirikishi ya TEHAMA ambayo ni muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa umma, kwani inaziwezesha Taasisi za Umma kushirikiana katika matumizi ya rasilimali za TEHAMA ili kuondoa urudufu, kupunguza gharama na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa umma na kuhakikisha usalama wa mawasiliano”, anafafanua Ndomba.

Naye, Meneja Usimamizi wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini kutoka e-GA Bw. Kulwa Kapama, anasema kuwa katika miaka mitatu ya uongozi wa Dkt. Samia, e-GA imewezeshwa na kufanikiwa kuboresha rasilimali shirikishi za TEHAMA kwakuweka Miundombinu salama ya TEHAMA.

Ametaja miundombinu hiyo kuwa ni Mkongo wa Taifa (NICTBB), Mtandao wa Serikali (GovNet), Vituo vya Kitaifa vya Data na Masafa ya Intaneti, inayoziwezesha Taasisi za Umma kushirikiana katika matumizi ya rasilimali za TEHAMA, ili kuondoa urudufu, kupunguza gharama na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa umma, pamoja na kuhakikisha uwepo wa usalama wa mawasiliano.

“Kutokana na uongozi bora wa awamu ya sita, Mamlaka imefanikiwa kujenga, kuboresha na kusimamia uendeshaji wa Vituo vya Serikali vya Kuhifadhi Mifumo na Taarifa (Government Data Center), ambapo hadi sasa vituo hivyo vinatumiwa na zaidi ya taasisi 121 kuhifadhi Mifumo na taarifa zao kwa usalama wa uhakika, ujenzi na usimamizi wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (GOVNET) ambapo hadi sasa Taasisi zaidi ya 299 zimeunganishwa na kuwezeshwa kuwasiliana chini ya uratibu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao”, anafafanua Bw. Kapama.

“Matumizi sahihi na salama ya TEHAMA, ni muhimu katika dunia ya sasa ili kupunguza mianya ya rushwa. kuboresha utoaji wa huduma kwa umma na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali”, hii ni moja ya kauli ya Mhe. Rais ambayo amekuwa akisisitiza dhamira yake ya kujenga Serikali ya kidijitali.

Katika kufikia malengo hayo, Mhe. Rais amekuwa akisisitiza uwepo wa mifumo ya TEHAMA ambayo inawasiliana na kubadilishana taarifa ili kuhakikisha utoaji wa huduma kwa wananchi unaimarika, ambapo e-GA imesanifu na kutengeneza Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji taarifa Serikalini ujulikanao ‘Government Enterprise Service Bus-GoVESB’

Aidha, Meneja wa Utengenezaji wa Mifumo ya TEHAMA wa e-GA Bw. Abdallah Samizi, anasema kuwa e-GA imeendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma kwa kutengeneza na kuboresha mifumo mbalimbali ya TEHAMA ukiwemo mfumo wa GoVESB.

Mfumo wa GoVESB, ni moja ya maelekezo ya Mhe. Rais ya kuhakikisha mifumo ya Serikali inawasiliana na kubadilishana taarifa lakini pia, ni utekelezaji wa Kifungu na. 48 cha Sheria ya Serikali Mtandao Namba. 10 ya Mwaka 2019 ambayo inaelekeza Mamlaka kutengeneza Mfumo shirikishi unao wezesha mifumo ya Taasisi za Umma kuwasiliana na kubadilishana taarifa.

Mamlaka kwa kushirikiana na taasisi nyingine za umma imesanifu na kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ikiwa ni Pamoja na Mfumo wa e-Mrejesho ambao unawawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Taasisi za umma kwa njia ya kidijitali, ili kuwasilisha maoni, mapendekezo, maswali, pongezi au malalamiko yao sambamba na kufuatilia utekelezaji wake ndani ya Taasisi husika.

“Mamlaka imetengeneza mfumo wa m-GOV, ambao ni mfumo jumuishi wa utoaji wa huduma za Serikali kwa njia ya simu za mkononi unaorahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma kwa umma, Mfumo huu umeunganishwa na watoa huduma wote wa simu za mikMononi nchini Tanzania na unatoa huduma za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwa kutoa na kupokea taarifa kupitia namba jumuishi 15200 na 15201 pamoja na huduma za menyu ya namba ya msimbo (USSD) kupitia namba jumuishi *152*00#”, anasema Bw. Samizi..

Mifumo mingine nipamoja na Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-office) unaorahisisha shughuli za mzunguko wa mafaili na nyaraka ndani ya Taasisi za Umma, Mfumo wa e-Board unaowezesha uratibu wa shughuli zote za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma.

Vilevile, Mfumo wa e-Mikutano unawawezesha watumishi wa Taasisi za Umma kufanya vikao kidijitali mahali walipo bila kulazimika kukutana mahali pamoja na hivyo kusaidia kupunguza gharama za uandaaji na uendeshaji wa vikao, mfumo e-Dodoso unaomuwezesha mwananchi au taasisi kutengeneza na kujaza dodoso, kupata tathmini pamoja na takwimu za dodoso kwa njia ya mtandao

Bi. Sultana Seiff Meneja Udhibiti wa Viwango vya TEHAMA anasema, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, Mamlaka imekuwa ikifanya vikao mbalimbali vya kiufundi na Taasisi za Umma kwa lengo la kutoa msaada, ushauri na elimu juu ya uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali Mtandao.

Aidha, takribani nyaraka zaidi ya 263 za TEHAMA zimewasilishwa kutoka Taasisi mbalimbali za umma ili kufanyiwa mapitio na kupata ushauri wa kiufundi na maboresho kupitia Tovuti ya Huduma za TEHAMA Serikalini (GISP) ambayo ni dirisha moja la huduma za TEHAMA Serikalini yenye lengo la kuhakikisha uwepo wa usimamizi bora wa miradi ya TEHAMA, utoaji wa huduma bora na ushirikishwaji wa taasisi za umma kwa ufanisi.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu ukomavu wa matumizi ya Teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index) uliofanyika mwaka 2022 katika nchi 198 duniani, inabainisha kuwa Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kushika nafasi ya 26 kidunia na ya pili barani Afrika nay a kwanza Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, mafanikio hayo yanatokana na utayari wa kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma, uwepo wa dira mahususi kuhusu sera ya TEHAMA, Sheria, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao, mikakati madhubuti na utekelezaji wake unaosimamiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).