Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-office) umetengenezwa ili kuwezesha na kurahisisha shughuli za utawala za kila siku ndani ya Taasisi za Serikali. Shughuli hizo zinahusu mzunguko wa mafaili na nyaraka ndani ya Taasisi za Umma.
Akieuelezea Mfumo huo Afisa TEHAMA wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Joseph Kimario alisema kuwa, Mfumo huu umekuwa ukifanyiwa maboresho madogo madogo ili kuuongezea ufanisi katika utendaji wake kuanzia toleo la kwanza na sasa maboresho yamefikia toleo la tano (Version 5), ambapo ufanisi wa Mfumo huu umekuwa ukiimarika kutoka toleo moja hadi jingine kadiri unavyofanyiwa maboresho.
“Ufanisi wa Mfumo hutofautiana kati ya toleo moja na jingine, kwa mfano katika toleo la nne la Mfumo huu kama barua ilitumwa kimakosa kwa mtu asiye husika Mfumo haukuruhusu kuituma tena barua hiyo hivyo, ilibidi kulifunga faili na kuanza kutuma upya, sasahivi kwenye toleo la tano Mfumo unaruhusu kama barua ilitumwa kimakosa kwa mtu asiye husika kupanga na kutuma upya kwa mtu anaye husika (re-assign) ili aweze kuendelea na utekelezaji” alisema Bw. Kimario.
Aidha, Bw. Kimario alisemakuwa toleo jipya (version 5) limeboreshwa mwonekano wake ili kumuwezesha Afisa anapoingia kwenye dashibodi kuona idadi ya barua alizonazo kwa ajili ya utekelezaji, zilizopo kwenye utekelezaji, zilizo pitisha muda wa utekelezaji (over due) pamoja na idadi ya barua ambazo Afisa husika amezishughulikia kwa siku, wiki na mwezi hivyo, kurahisha upatikanaji wa ripoti.
Maboresho mengine ambayo yamefanyika kwenye Mfumo huo toleo la 5 ni wepesi (lightness) katika kutafuta mafaili na barua zilizoshughulikiwa kipindi cha muda mrefu tofauti na toleo la 4 ambalo lilikuwa linachukua muda mrefu kidogo hasa wakati wa kutafuta mafaili au barua za zamani.
“Kwenye toleo la 4 la Mfumo wa Ofisi Mtandao kipengele kimoja cha Mfumo ‘Component’ kikishindwa kufanya kazi, Mfumo mzima uliathirika na kushindwa kufanya kazi ipasavyo lakini toleo la 5 limeboreshwa na kuweza kutofautisha ‘back end’ na ‘front end’ ya Mfumo hivyo, kipengele kimoja kisipofanya kazi hakiathiri utendaji kazi wa Mfumo wote”, alifafanua Bw. Kimario.
Mfumo wa Ofisi Mtandao unapatikana kupitia https://eoffice.gov.go.tz kwa Taasisi zote za Umma zilizounganishwa kwenye Mtandao wa Mawasiliano ya Serikali (GOVNET) kwa kutumia anuani rasmi ya Baruapepe ya Serikali (GMS).
Mfumo huu ni mzuri kwani unahakikisha usalama wa uhakika wa taarifa, data na majalada ya Serikali na hupatikana kwa watumishi wa Serikali waliopo ofisini au waliunganishwa na VPN ya Serikali tu. Toleo la 5 la Mfumo wa Ofisi Mtandao lilianza kutumika Disemba Mosi Mwaka huu.