emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MFUMO WA NGAO KUIMARISHA ZAIDI USALAMA WA MIFUMO YA TEHAMA SERIKALINI


MFUMO WA NGAO KUIMARISHA ZAIDI USALAMA WA MIFUMO YA TEHAMA SERIKALINI


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imetengeneza Mfumo wa Usalama wa Kidigitali wa Uthibitishaji wa vipengele vingi ujulikanao kama NGAO, utakaotumika kuhakikisha usalama wa ziada wa taarifa muhimu kwa watumiaji wa mifumo ya Serikali.

Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa TEHAMA Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Sylvani Shayo amesema, mfumo wa NGAO unalenga kuhakikisha watumiaji wanaweza kufikia mifumo ya Serikali kwa njia salama zaidi, kupunguza hatari za udukuzi na matumizi mabaya ya taarifa za serikali.

Bw. Shayo ameeleza kuwa, mfumo wa NGAO unatumia programu ya ‘NGAO Authenticator’ inayotengeneza nenosiri (nywila) ya mara moja (One-Time Password - OTP), kwa kila uthibitisho wa mtumiaji ambayo itasaidia kuimarisha usalama wa watumiaji kwa kutoa tabaka lingine la ulinzi zaidi ya baruapepe ya mtumiaji na nenosiri.

“ Kila mtumiaji wa mifumo ya TEHAMA, hupaswa kuweka baruapepe anayotumia na nenosiri kila anapotaka kuingia kwenye mfumo, hii ni hatua ya awali na ya kawaida lakini kupitia mfumo huu wa NGAO kutakuwa na hatua ya pili baada ya kuingia kwenye mfumo, mtumiaji atahitaji kuthibitisha utambulisho wake kwa kutumia njia nyingine, kama vile kupitia ujumbe mfupi (SMS) kwenye simu yake ya kiganjani”, amesema Shayo.

Amebainisha kuwa, mfumo wa NGAO utasaidia kupunguza hatari za udukuzi kupitia njia za kawaida za nenosiri kwa kuhitaji uthibitisho wa ziada pamoja na kujenga uaminifu wa watumiaji kwakuwa taarifa zao zinahifadhiwa kwa usalama na zinaweza kufikiwa tu na watu waliothibitishwa.

“Umuhimu wa NGAO ni mkubwa sana katika kulinda taarifa nyeti za Serikali na kutoa mazingira salama kwa watumiaji wa mifumo ya Serikali na hivyo kumuwezesha anayehusika tu na taarifa hizo kuweza kuzifikia” amesisitiza Shayo.

Ameongeza kuwa, mfumo huo unawawezesha watumiaji wa mifumo ya Serikali kupokea taarifa kwenye simu zao za kiganjani kila wanapojaribu kuingia kwenye mfumo, na kupewa nafasi ya kukubali au kukataa ombi la kuingia, lakini pia kupokea taarifa za uthibitisho kwenye laini za simu bila hitaji la mtumiaji kuwa na mtandao wa intaneti.

Kwa sasa, mfumo wa NGAO unatumiwa kwa majaribio na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) pekee katika Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) na Mfumo Shirikishi wa Kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi (ERMS), huku malengo yakiwa ni kuongeza matumizi ya mfumo huo katika mifumo mingine ya Serikali ili kuhakikisha usalama wa taarifa na kuimarisha ufanisi katika shughuli za Serikali Kidijitali.