Kutokana na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika karne hii ya 21, matumizi ya simu za mkononi yameendelea kuongozeka ambapo, kwa sasa simu zinatumika kwa matumizi mengine mengi zaidi na si kwa ajili ya mawasiliano pekee kama ilivyokuwa hapo awali.
Pamoja na kuongezeka kwa aina mbalimbali ya matumizi hayo, lakini pia simu imekuwa ni kifaa na kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi kwani, simu hutumiwa na Serikali kutoa huduma na kuwawezesha wananchi kupokea huduma hizo kidijitali kupitia simu ya mkononi mahali walipo.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Serikali kwa urahisi zaidi, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imetengeneza Mfumo wa Kutoa Huduma za Serikali kupitia Simu za Mkononi (mGov), wenye lengo la kuziwezesha taasisi za umma kuwahudumia wananchi kwa urahisi, uharaka, usalama na gharama nafuu kupitia simu zao za mkononi.
Aidha, mfumo huu umejumuisha huduma mbalimbali za Serikali na unatumia arafa (SMS) katika kutoa na kupokea taarifa ikiwemo SMS za ununuzi wa umeme (LUKU), SMS za huduma za malipo ya Serikali (GePG), huduma za kikodi (TRA), huduma za ardhi, huduma za afya (NHIF, CHF), huduma za kilimo, ajira, maji, elimu, sheria, haki, uwasilishaji wa maoni au mrejesho n.k.
Kutokana na mabadiliko ya teknolojia pamoja na maoni mbalimbali ya watumiaji wa mfumo wa m-GOV, e-GA iliamua kufanya maboresho katika mfumo huo kutoka mGov nakuwa mGov 2.0, kwa kuuongezea mfumo ufanisi zaidi katika utendaji kazi wake.
Kaimu Meneja wa Sehemu ya Huduma za Serikali kupitia Simu za Mkononi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Aziz Abdulaziz amesema kuwa, Mamlaka iliamua kufanya maboresho kwenye mfumo huo ili uweze kuendana na wakati na kuhimili mabadiliko ya teknolojia pamoja na kuwa bora zaidi katika usalama wake.
“Awali Taasisi za Umma zilipokuwa zikihitaji kutengenezewa jina la mtumiaji (white listing of SenderID) ilizillazimu taasisi kutuma maombi yake e-GA na baada ya kupokelewa, yalitumwa kwa watoa huduma kwa ajili ya utekelezaji na kisha taasisi hizo zilitakiwa kufanya ufuatiliaji wa majibu ya ombi husika, ili kujua kama ombi limekamilika au bado, baada ya maboresho ya mGov 2.0, sasa taasisi inaweza kufuatilia utekelezaji wa ombi lake kupitia mfumo”, amesema Aziz.
Ameongeza kuwa, mfumo wa mGov 2.0 unaruhusu ujazaji wa dodoso kupitia simu za mkononi kwa njia ya sms, ambapo taasisi husika huandaa dodoso na kutuma kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) kwa wahusika, na ili mtu aweze kujaza dodoso hilo ni lazima ajiunge (subscribe), ndipo atatumiwa maswali yanayoambatana na majibu mbalimbali ambayo mjazaji wa dodoso atachagua jibu analodhani ni sahihi kwake, amefafanua Azizi.
Aidha, amebainisha kuwa, mfumo huu umewezeshwa na kuongezewa uwezo wa kuruhusu utumwaji wa ujumbe wa maandishi kwa ajili ya kujulisha jambo fulani kwa walengwa (notification sms).
“Kwenye mfumo wa mGov hapo awali mtu akiwa nje ya nchi alikuwa hawezi kupokea sms zinazotumwa kupitia mfumo, lakini baada ya kukamilika maboresho ya mGov 2.0 arafa (sms) zitaweza kutumwa nje ya nchi, na hii itasaidia sana kwa watu wanaofuatilia zabuni mbalimbali pamoja na mambo ya uwekezaji ambao wapo nje ya nchi,” amesema Aziz.
Ameongeza kuwa, mfumo wa mGov 2.0 utaunganishwa na mfumo wa baruapepe Serikalini (GMS), ambapo utaziwezesha taasisi zinazoutumia mfumo huu ziweze kutuma baruapepe na ujumbe huo ukapokelewa kama ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu ya mkononi.
“Kwasasa tupo katika hatua za mwisho za kuwezesha matumizi ya mwitiko wa sauti (Interactive Voice Response) ambapo taasisi zinazotumia mfumo huu, zitakuwa na uwezo wa kuwafikishia huduma wananchi kwa njia ya sauti ambapo itakuwa msaada mkubwa kwa watu wenye changamoto ya kuona pamoja na wale wasiojua kusoma”, amefafanua Azizi.
Akilezea faida za maboresho yaliyofanyika kwenye mfumo huo, Afisa TEHAMA sehemu ya Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mkononi Bi. Erna Mwende, amesema kuwa usalama wa taarifa na takwimu zote umeimarika kwani teknolojia iliyotumika katika mGov 2.0 ni mpya na inaweza kutambua viashiria hatarishi vyote vya kiusalama.
Erna amesema kuwa, mGov 2.0 katika utendaji kazi wake imezigawanya moduli zake zilizopo kwenye mfumo (push sms, pull sms n.k), hivyo eneo moja linapokuwa na changamoto au linapokuwa katika hali ya kufanyiwa maboresho halitoathiri utendaji kazi wa moduli nyingine.
Amebainisha kuwa, awali upatikanaji wa ripoti uliilazimu taasisi husika kuwasiliana na e-GA ili kuweza kupata ripoti mbalimbali, lakini kwa sasa mfumo unatoa ripoti wenyewe na mtumiaji wa mfumo anaweza kupangilia kwenye mfumo atumiwe ripoti zipi na kwa njia gani kulingana na matakwa ya taasisi yake.
Aziz amesema kuwa, matarajio ya baadaye ni kuuwezesha mfumo huo uwe rafiki zaidi ili kila Tasisi ya Umma iweze kujihudumia yenyewe ndani ya mfumo bila kuhitaji msaada wa mtu mwingine ili kuepusha mianya inayoweza kuleta urasimu.
Mfumo wa mGov 2.0 umeunganishwa na watoa huduma wote wa simu za mkononi nchini Tanzania ambao ni TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo/Zantel na Halotel, mfumo unatoa huduma za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kupitia namba jumuishi 15200 na 15201 pamoja na huduma za menyu ya USSD kupitia namba jumuishi *152*00#, na unaziruhusu Taasisi za Umma kutoa huduma kupitia namba binafsi za taasisi, kama vile *113# ya PCCB inayotoa huduma ya kuripoti matukio ya rushwa.