emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MFUMO WA GMS WARAHISISHA MAWASILIANO SERIKALINI


MFUMO WA GMS WARAHISISHA MAWASILIANO SERIKALINI


Mawasiliano kwa njia ya baruapepe ‘email’, yameendelea kushika hatamu duniani ikiwa ni miongoni mwa njia ya haraka ya mawasiliano inayotumika katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za taasisi.

Kukua kwa matumizi ya baruapepe, kunatokana na ukuaji wa teknolojia na hivyo, kuwa ni moja ya njia ya haraka na inayoaminika katika mawasiliano rasmi ya kiofisi.

Ili kuhakikisha Serikali inapiga hatua katika matumizi ya baruapepe, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imetengeneza Mfumo wa baruapepe Serikalini (Government Mail System - GMS), ili kurahisisha mawasiliano na kubadilishana taarifa ndani na nje ya Serikali kwa uhakika na usalama zaidi.

Meneja wa Utengenezaji wa Mifumo ya TEHAMA wa e-GA Bw. Abdallah Samizi alisema, e-GA ilitengeneza mfumo wa GMS mwaka 2013 ili kuhakikisha Serikali inakuwa na mfumo salama na wa uhakika katika mawasiliano yake.

“Awali, kabla ya kuwepo kwa mfumo huu wa GMS, taasisi za Serikali zilitumia mifumo yake binafsi iliyotengenezwa na wakandarasi au baruapepe za muda mfupi ‘disposable email’ kama Yahoo na Gmail kubadilishana taarifa na nyaraka mbalimbali za Serikali”, alifafanua Bw. Samizi.

Alibainisha kuwa, mifumo hiyo ilikuwa ikifanya kazi kwa kusuasua kutokana na changamoto mbalimbali za kimiundombinu na pia haikuwa salama kwasababu hakuna uhakika wa mahali zinapotunzwa taarifa kwani hakuna makubaliano na Serikali.

Aidha, aliongeza kuwa gharama za ununuzi na uendeshaji wa mifumo hiyo ya baruapepe zilikuwa kubwa na ufanisi wake ulikuwa mdogo, changamoto ambazo zimetatuliwa kupitia mfumo wa GMS ambao umeimarisha usalama wa taarifa za Serikali na uhakika wa upatikanaji wa huduma ya baruapepe.

“GMS ina usalama wa kutosha kwa kuhakikisha mawasiliano yote kwa njia ya baruapepe yanahifadhiwa na kubaki kwenye miundombinu ya Serikali na hivyo kuwa na uhakika wa usalama wa taarifa za Serikali”, alisisitiza Bw. Samizi.

Aliongeza kuwa, mfumo wa GMS ni shirikishi na unawezesha mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa na nyaraka baina ya taasisi moja na nyingine, hivyo kuipunguzia Serikali gharama za ununuzi na uendeshaji wa mifumo ambapo awali Serikali ilitumia fedha nyingi katika kuhudumia mifumo mbalimbali ya baruapepe katika taasisi za umma.

“Taasisi za Umma zinatumia rasilimali shirikishi katika kuendesha mfumo huu ikilinganishwa na hapo awali ambapo, kila taasisi ya umma ilijaribu kutengeneza mfumo wake wa kipekee uliotumia gharama nyingi za uendeshaji na haikufanya kazi kwa ufanisi wala kukidhi mahitaji halisi ya mtumiaji”, alisema Bw. Samizi.

Alibainisha kuwa, mfumo wa GMS ni wa kuaminika kwani umetengenezwa nchini na wataalamu wa ndani, hivyo taarifa na nyaraka mbalimbali za Serikali zinapotumwa hazitoki nje ya Tanzania.

Alisisitiza kuwa, taarifa zinazotumwa kupitia GMS zinahifadhiwa mahali salama kwenye vituo vya Serikali vya kuhifadhi mifumo na taarifa na hivyo kudumisha usiri wa taarifa hizo na kulinda maslahi mapana ya taifa.

“Tofauti na mifumo mingine ya baruapepe, mfumo huu wa baruapepe Serikalini (GMS) umeunganishwa na mifumo mingine na hivyo kurahisisha utumiaji wa mifumo mingine ndani ya Serikali”, alisema Bw. Samizi na kuongeza kuwa,

“Mfumo wa GMS umeendelea kuboreshwa kila wakati kulingana na mabadiliko ya ukuaji wa teknolojia yanayojitokeza mara kwa mara ili kukidhi viwango stahiki vya mifumo ya baruapepe duniani”.

Bw. Samizi alibainisha kuwa, matumizi ya mifumo ya baruapepe isiyo ya Serikali inahatarisha usalama wa taarifa za Serikali na hivyo, ni wajibu wa watumishi wa umma kulinda usalama wa taarifa za Serikali kwa kufanya mawasiliano na kutuma nyaraka za Serikali kupitia GMS.

Hadi sasa taasisi za umma 690 zinatumia mfumo huu wa GMS katika mawasiliano ya kiofisi kwa usalama na uhakika, pia mfumo huu unatoa fursa kwa taasisi za umma, kuweka matangazo na matukio mbalimbali ya kitaifa kwenye ukurasa wa mbele wa mfumo huu tofauti na mifumo mingine ya barua pepe.