emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MAZINGIRA WEZESHI YATAJWA KUCHOCHEA UKUAJI WA SERIKALI MTANDAO


MAZINGIRA WEZESHI YATAJWA KUCHOCHEA UKUAJI WA SERIKALI MTANDAO


Uwekezaji katika rasilimali watu, miundombinu, fedha, sera na sheria ya Serikali Mtandao umetajwa kuwa kichocheo katika jitihada za ujenzi wa Serikali Mtandao na kurahisisha utendaji kazi Serikalini pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa jana (09/09/2024) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwenye ufunguzi wa Kongomano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki linalofanyika katika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.

Ndomba alisema kuwa, Serikali imeendelea kuwekeza katika jitihada za Serikali Mtandao kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo sheria, rasilimali watu, fedha na miundombinu na hivyo kuleta mafanikio makubwa yakiwemo usanifu wa mifumo mikubwa jumuishi na ya kimkakati inayotumika katika taasisi mbalimbali za Serikali.

“Serikali ya awamu ya sita, imeweka mazingira wezeshi kwetu sisi e-GA ambao tumepewa dhamana ya kusimamia TEHAMA Serikalini, ikiwa ni pamoja na kupata fedha za uendeshaji wa taasisi na miradi mikubwa ya TEHAMA ya kitaifa, kupata mafunzo ya mara kwa mara ya kuwajengea uwezo Maafisa TEHAMA pamoja na mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao”, alisema Ndomba.

Kutokana na uwekezaji huo, e-GA kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma imefanikiwa kujenga na kusanifu mifumo muhimu ya kitaifa ikiwemo Mfumo wa Kusimamia Malipo ya Serikali (GePG), Mfumo Jumuishi wa Malipo ya Papo Hapo (TIPS), Mfumo wa Uondoshaji Shehena maeneo ya Forodha (TeSWS), Mfumo wa Barua Pepe za Serikali (GMS) na Mfumo wa Ajira Serikalini (Ajira Portal), alisema Ndomba.

“Mifumo mingine ni ule wa Kusimamia Rasilimaliwatu (HCMIS), Mfumo wa Kusimamia Rasilimali za Maji na Utoaji wa Ankara za maji (MAJIIS), Mfumo wa Kusimamia Utoaji wa Huduma za Serikali kwa Njia ya Simu za Mkononi (mGOV), pamoja na Mfumo wa Kusimamia Ununuzi wa Umma (NeST)”, alifafanua Ndomba.

Sambamba na hilo, Ndomba ametoa rai kwa taasisi za umma kujiunga katika Mfumo Mkuu wakubadilishana Taarifa Serikalini (Government Enterprise Service Bus – GovESB), ili ziweze kubadilishana taarifa kidijitali kama ambavyo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akielekeza taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijiti.

“Ili kuwa na Serikali Mtandao madhubuti, ubadilishanaji taarifa kidijitali ni kiungo muhimu hivyo nitumie nafasi hii kutoa rai kwa taasisi ambazo bado hazijajiunga na mfumo wa GovESB kutekeleza maelekezo ya Mh. Rais kwa kujiunga na mfumo huu ili ziweze kubadilishana taarifa kidijitali ” alisisitiza Ndomba.

Amebainisha kuwa, hadi sasa taasisi za umma 164 zimeshaunganishwa, na Mifumo 159 inabadilishana taarifa kupitia mfumo huu wa GovESB, miongoni mwa taasisi hizo ni Taasisi za Haki Jinai (Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa -TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka - NPS na Mahakama).

Kongomano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki linafanyika kwa siku nne (04) Kuanzia Septemba 09 – 12 mwaka huu jijini Arusha, ambapo e-GA ni miongoni mwa wadhamini wa kongamano hilo.