emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

MATUMIZI YA MFUMO WA E-MREJESHO NI TAKWA LA KISHERIA: UTUMISHI


MATUMIZI YA MFUMO WA E-MREJESHO NI TAKWA LA KISHERIA: UTUMISHI


Taasisi zote za Umma zatakiwa kujiunga na kutumia mfumo wa e-Mrejesho ili kuweza kutatua changamto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi wakati akifunga kikao kazi cha mafunzo ya mfumo wa e-Mrejesho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa Oktoba4, 2024.

"Kabla ya mwezi huu Oktoba kuisha taasisi zote za Umma ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo wa e-Mrejesho zianze kuutumia mfumo huu na kuhakikisha kero zote zinazowasilishwa ndani ya mfumo zinafanyiwa kazi"amesema Daudi.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema kuwa matumizi ya mfumo wa e-Mrejesho ni takwa la kisheria na sio maamuzi ya taasisi kutumia au kutotumia mfumo huo kwani kwakutokushughulikia kero zinazowasilishwa nikuwanyima wananchi haki za msingi.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo ametaka viongozi wa taasisi zote za Umma kuhakikisha wanaimarisha dawati la mrejesho kwakuweka watumishi wenye weledi na wanaoweza kutunza siri.

Vilevile amewataka viongozi wa Taasisi za Umma kuhakikisha maofisa mrejesho wote wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali zinazo wasilishwa kwenye dawati hilo la mrejesho.

Akishukuru kwaniaba ya washiriki wote Mwenyekiti wa kikao kazi hicho Bw. Fadhili Sultani amesema kuwa anaishukuru Ofisi ya Rais - Utumishi pamoja na e-GA kwa kuandaa mafunzo hayo.

Aidha, Mwenyekiti huyo ameomba hoja zote zilizowasilishwa kwa ajili ya kufanyiwa maboresho zifanyiwe kazi mapema na zinapokamilika wapate fursa ya kuupitia mfumo huo kabla haujaanza kutumika rasmi.

Sultani pia ameomba watumishi wa taasisi nyingine ambao hawajapata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo wapatiwe nafasi ya kupitishwa kwenye mfumo huo ili waweze kutoa maoni yao.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Udhibiti na Usalama wa Mifumo ya TEHAMA wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Silyvan Shayo amesema e-GA ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Rais - Utumishi na kuhakikisha maboresho yoye yanafanyiwa kazi kwa wakati kama wadau walivyoomba.

Aidha, Shayo amesema kuwa mfumo wa e-Mrejesho unafanya kazi kwa ufanisi na unapatikana wakati wote kupitia simu za mkononi *152*00#, aplikesheni tumizi ya e-Mrejesho au tovuti www.emrejesho.gov.go.tz

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Bi . Leila Mavika, Mkurugenzi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kuwa kundi hili la kwanza la maafisa waliopatiwa mafunzo hayo ni Maafisa Mrejesho na TEHAMA wapatao 105 ambao taasisi zao zinafanya vizuri katika kutumia mfumo wa e-Mrejesho.