Matumizi ya mfumo wa kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika halmashauri na Taasisi za Umma (e-Board), yameiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuokoa zaidi ya shilingi milioni 160, zilizokuwa zikitumika katika ununuzi wa vifaa mbalimbali vya uchapishaji na uaandaaji wa muhtasari wa vikao kila mwaka.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Bw. Elias Mahwago Kayandabila, ofisini kwake mjini Tabora wakati akieleza faida walizozipata mara baada ya kuanza kutumia mfumo huo.
“Mfumo wa e-Board umetusaidia kukoa fedha nyingi tulizokuwa tukitumia kuwalipa waendesha vikao kwaajili ya kusambaza makabrasha kwa madiwani pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumika katika uandishi wa vikao kila mwaka”, alisema Bw. Kayandabila.
Alieleza kuwa, Manispaa ya Tabora imeanza kutumia mfumo wa e-Board Julai 2023, na tangu wakati huo imepata faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ufanisi wa uendeshaji wa vikao na kuokoa gharama, kwani kila mwaka Manispaa hiyo ilikuwa ikitumia zaidi ya shilingi Milioni 160 kwa ajili ya kulipa makarani pamoja na ununuzi wa vifaa mbaimbali.
Aidha, Kayandabila alioa rai kwa halmashauri zote nchi ambazo hazijaanza kutumia mfumo wa e-Board katika uendeshaji wa shughui zao zianze kutumia mfumo, huo kwani utawasaidia katika kuongeza ufanisi na kuokoa gharama za uendeshaji.
‘’Sisi tulianza kutumia mfumo wa e-Board ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia na kwakweli tumeona manufaa makubwa sana, ukilinganisha hapo awali, hivyo niziombe halmshauri nyingine zisiogope kuingia kwenye matumizi ya TEHAMA kwani hawatajutia’’, alisistiza.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe Ramadhani Shabani Kapela, alisema kwa kutumia mfumo wa e-Board mpaka sasa wamekwishafanya vikao tisa (9) vya kamati ya fedha, vikao 32 vya kamati za kawaida, vikao viwili (02) na mabaraza ya madiwani matatu (3) na kwa kipindi chote hicho hawajawahi kupata changamoto yoyote katika mfumo.
‘’Matumizi ya mfumo huu ni jambo la kujivunia sana kama Manispaa, sisi tumekuwa tukiutumia mfumo huu karibu mwaka mzima sasa, mwanzo madiwani walipata tabu kidogo kulingana na ugeni wa matumizi ya vishikwambi, lakini kwa sasa kila mmoja anaufurahia kwani hatujawahi kupata changamoto yoyote’’Alisema
Naye Hussein Masoud Luziga ambaye ni mwandishi wa vikao na mikutano katika Manispaaa ya Tabora alisema, hapo awali walikuwa wakipata usumbufu mkubwa katika uandaaji wa muhtasari na usambazaji wa taarifa za kikao, lakini mara baada ya kuanza kutumia mfumo wa e-Board, wamekuwa wakiweka taarifa zote ndani ya mfumo hivyo umeondoa usumbufu wa kuzunguka kusambaza makabrasha kwa madiwani na wajumbe wa vikao vya Bodi
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ikomwa manispaa ya Tabora Mhe. Salum Magembe alisema, mfumo wa e-Board umemuwezesha kuhudhiria vikao vya Baraza hata kama yuko nje ya Manispaa, huku Diwani wa viti maalumu katika Manispaa hiyo Mhe. Marry Bisambi akiipongeza e-GA kwa kubuni mfumo huo ambao wao kama madiwani wa halmshauri ya Tabora wameupokea vizuri kutokana na wingi wa faida zake.
Mfumo wa e-Board ni mfumo uliotengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa ajii ya kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya Bodi na Menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za umma