emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mamlaka ya Serikali Mtandao Yatekeleza Agizo la Rais


Mamlaka ya Serikali Mtandao Yatekeleza Agizo la Rais


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza Mamlaka ya Serikali Matandao (eGA) kwa kutengeneza mfumo utakaowezesha mifumo mbalimbali ya Serikali kubadilishana taarifa, jambo hili ni hatua kubwa katika utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA ndani ya Serikali inawasiliana na kubadilishana taarifa wakati wowote.

Akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo jijini Dodoma, Waziri Mhagama amefurahishwa na utekelezaji wa haraka wa agizo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inayotumiwa ndani ya Serikali inawasiliana na kubadilishana taarifa ili kurahisisha utoaji huduma kwa umma.

“Ninatoa pongezi nyingi kwa Mamlaka kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais kwa wakati na ninafahamu kuna baadhi ya taasisi za umma zimeshaunganishwa katika mfumo huo, hivyo ninaagiza kazi ya kuunganisha taasisi zilizobaki ikamilike kwa wakati na kufanya kazi kama ilivyodhamiriwa” Alisema Mhe.Mhagama.

Aidha, Mhe. Mhagama ametoa wito kwa watanzania kuendelea kutumia mifumo ya TEHAMA iliyobuniwa, kusanifiwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani katika shughuli zao za kila siku kwani zinarahisisha sana utendaji kazi, kupunguza gharama na mianya ya rushwa.

Pia, Mhe. Mhagama amesisitiza na kuwataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa kufuata maadili ya Utumishi wa Umma hasa wanapotumia mifumo ya kidijitali kwa uzalendo na uwajibikaji ili kumsaidia Mhe. Rais katika kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi kama kaulimbiu ya awamu ya sita ya “Kazi Iendelee” inavyosadifu.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Benedict Benny Ndomba amesema katika utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais, Mamlaka imetengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (MUTAS) ambao mpaka sasa umeunganisha na unatumiwa na taasisi kumi kwa hatua ya majaribio.

Katika taarifa yake, Mhandisi Ndomba ameainisha baadhi ya mifumo mingine iliyotengenezwa na eGA kwa kushirikiana na taasisi husika na kwa kutumia wataalamu wa ndani kuwa ni Mfumo wa Ukusanyaji Malipo ya Serikali Kielektroni (GePG) unaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, Mfumo wa Pamoja wa Utoaji Ankara kwa Mamlaka za Maji nchini (MAJIIS) unaosimamiwa na Wizara ya Maji, Mfumo wa Kusimamia Rasilimaliwatu Serikalini (New HCMIS) unaosimamiwa na Ofisi ya Rais Utumishi, Mfumo wa kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi (ERMS), Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) na Mfumo wa Baruapepe Serikalini (GMS).

Ziara hiyo ya Waziri Mhagama kwenye Ofisi ya Mamalaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma iliyofanyika Februari 11, 2022 ni sehemu ya kuzitambua taasisi zote zilizopo chini ya Wizara yake ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.