Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na Chuo Kikuu Mzumbe, wamesaini hati ya makubaliano (MOU) ya ushirikiano katika masuala ya elimu, utafiti, na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha na kukuza tasnia ya TEHAMA ili kuboresha jitihada za Serikali Mtandao sambamba na kuimarisha uhusiano uliopo katika taasisi hizo.
Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, imefanyika hivi karibuni katika ofisi za Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, na kushuhudiwa na baadhi ya watumishi wa taasisi zote mbili pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Uwezeshaji e-GA, CPA. Salum Mussa, alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kuongeza tija katika kukuza na kuimarisha tasnia ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi wa tasnia hiyo wa Chuo Kikuu Mzumbe kujifunza kwa vitendo kupitia program maalum inayotolewa na e-GA katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC).
“Pamoja na fursa hiyo kwa wanafunzi, pia ushirikiano wetu na Chuo Kikuu Mzumbe utaimarika zaidi na tunatarajia bunifu nyingi za TEHAMA zitaibuliwa kupitia Kituo chetu cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC), kwakuwa tutapata nafasi ya kushirikiana na wataalamu katika tafiti na bunifu mbalimbali kutoka Chuo Kikuu Mzumbe”, alisema Bw. Salum.
Alifafanua kuwa, Mamlaka imedhamiria kuwaleta wataalamu na watafiti mahiri katika masuala ya TEHAMA kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, ikiwa ni pamoja na Madaktari na Maprofesa wa masuala ya TEHAMA, ili kushirikiana nao kwenye miradi ya bunifu inayozalishwa katika kituo hicho, ambapo wataalamu hao wataweza kutoa ushauri wa namna ya kutatua changamoto mbalimbali ili kuwa na Serikali Mtandao yenye tija.
Naye, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwagoha, alisema kuwa makubaliano hayo yanaweka msisitizo mkubwa kwenye masuala ya ufundishaji na utafiti ili kuhakikisha wanafunzi wa TEHAMA katika chuo hicho wanajengewa uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka kwa maendeleo ya taifa letu.
"Tunaangazia kuboresha jinsi tunavyotoa elimu kwa wanafunzi wetu wa fani ya TEHAMA, kwa kuwa ushirikiano huu utasaidia kuonesha maeneo ambayo tunatakiwa kuweka msisitizo au kuboresha zaidi ili kuwa na wataalamu wazuri kwenye eneo la TEHAMA, lakini pia itasaidia chuo kuwa na programu zaidi za elimu kwa njia ya mtandao.," alisema Profesa Mwagoha.
Profesa Magoha alibainisha kuwa, utafiti utakuwa eneo muhimu la ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na e-GA, ambapo Watafiti kutoka e-GA watashirikiana na wenzao wa chuo hicho katika kutatua changamoto za kiteknolojia na kubuni mifumo ya TEHAMA inayoweza kutumika Serikalini ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.