Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), inatarajia kufanya kikao kazi cha nne (4) cha Serikali Mtandao Februari 6 hadi 8, mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dodoma, Meneja Mawasiliano wa e-GA Bi. Subira Kaswaga amesema, lengo la kikao kazi hicho ni kuwakutanisha wadau wa Serikali Mtandao kutoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma, ili kujadili jitihada mbalimbali za utekelezaji wa Serikali Mtandao na kuweka mikakati itakayosaidia kukuza na kuimarisha Serikali Mtandao nchini.
Subira amesema kuwa, kikao hicho kitaongozwa na kauli mbiu isemayo “Uzingatiaji wa Sheria, Sera, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa ubadilishanaji Salama wa Taarifa”.
“Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji huduma kwa umma, lakini pia ili hili liweze kutokea ni lazima tuwe na mifumo ambayo imetengenezwa kwa kuzingatia Sheria, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao”, amesema Subira.
Ameongeza kuwa, takriban wadau 1,000 wa Serikali Mtandao kutoka katika mashirika na taasisi mbalimbali ya umma wanatarajiwa kushiriki kikao hicho wakiwemo Maafisa Masuuli, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA, Maafisa TEHAMA na watumiaji wengine wa mifumo ya TEHAMA.
Aidha, Subira amesema kuwa, katika kikao hicho mada mbalimbali zinazohusu Serikali Mtandao zitawasilishwa sambamba na kupata taarifa ya utekelezaji wa maazimio 12 yaliyofikiwa katika kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao kilichonyika Februari mwaka jana.
“Mwaka jana tulifanya kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao na kuweka maazimio 12 ambayo yaliwekwa na washiriki wa kikao hicho, hivyo mwaka huu tutawasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo ni wakati mzuri kwa washiriki kufahamu yale waliyokubaliana na kufahamu utekelezaji wake”, amefananua Subira.
Aidha, Subira ametoa rai kwa wadau wote wa Serikali Mtandao nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kikao kazi hicho na kujisajili kupitia mfumo wa mafunzo na semina (TSMS) unaopatikana kwa kikoa cha www.tsms.ega.go.tz.