emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

JIFUNZENI TEKNOLOJIA MPYA KWA MASLAHI YA TAIFA: NDOMBA


JIFUNZENI TEKNOLOJIA MPYA KWA MASLAHI YA TAIFA: NDOMBA


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi, Benedict Ndomba, amewataka wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo na mafunzo kazini katika fani ya TEHAMA, kutumia fursa hiyo kujikita zaidi katika kuzielewa teknolojia mpya zinazoibukia ili kuhakikisha zinaleta tija kwa Taifa.

Ndomba ameyasema hayo leo jijini Dodoma, wakati akifungua programu ya mafunzo kwa vitendo (practical training) pamoja na mafunzo kazini (internship) kwa mwaka wa fedha 2024/2025, inayoendeshwa na Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC).

“Teknolojia mpya zinaibuka kila mara duniani, hivyo mnapokuwa hapa mtumie nafasi hii kujifunza na kubuni vitu vipya kadri mabadiliko ya teknolojia yanavyojitokeza, lakini ni lazima muhakikishe vitu vyote mnavyobuni vinakuwa na maslahi mapana kwa Taifa” amesema Ndomba.

Ameeleza kuwa, e-GA kupitia e-GovRIDC imekuwa ikiendesha mafunzo hayo kila mwaka kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa fani ya TEHAMA kutoka vyuo mbalimbali kupata ujuzi na uzoefu pamoja na kufahamu hali ya soko la ajira ilivyo ili waweze kushindana katika soko la ajira kimataifa.

“Kwa upande wa mafunzo kazini ‘Internship’ na nafasi za wanaojitolea, tunao watumishi waliosoma ndani na nje ya nchi, kituo hiki kinatoa nafasi kwa Mtanzania yeyote aliyepo ndani na nje ya nchi mwenye shauku ya utafiti na ubunifu kuwasilisha maombi yake kupitia mfumo wa Ubufuni (ubunifu.ega.go.tz)”, amefafanua Ndomba.

Ameongeza kuwa, madhumini ya e-GovRIDC ni kufanya tafiti kwenye eneo la Serikali Mtandao na TEHAMA kwa ujumla sambamba na kuwajengea uwezo vijana wazawa kupitia programu mbalimbali zikiwemo za mafunzo kwa vitendo, mafunzo kazini na nafasi za kujitolea kwa kushirikiana na Vyuo vya Elimu ya Juu Nchini na Nje ya nchi.

Aidha, Ndomba amewataka vijana hao kutumia teknolojia mpya katika kubuni mifumo itakayoongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini na kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali kwa wananchi.

“Ni matarajio yangu kuwa kila mmoja wenu atashiriki kikamilifu katika kuzielewa na kuzitumia teknolojia hizi kwakuwa huu ndio uelekeo wa dunia sambamba na hilo mtaweza kubuni mifumo mbalimbali kupitia teknolojia hizo”, amesema Mhandisi Ndomba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji wa e-GA Bw.Salum Mussa, amewapongeza vijana hao kwa kupata fursa ya kushiriki katika programu hiyo na kuwataka kutumia fursa hiyo kupata ujuzi na uzoefu utakaowasaidia kufanya vema zaidi watakaporejea vyuoni.

Aidha, Meneja wa eGovRIDC Mhandisi. Dkt. Jaha Mvulla, amesema kuwa mafunzo hayo kwa mwaka huu yamejikita zaidi katika kuzielewa teknolojia mpya zinazoibukia ‘Emerging Technology’ kama vile Akili Bandia ‘Artificial Intelligence’, Sarafu ya Kidijitali ‘Digital Currency’, Block Chain, Usalama wa Mtandao ‘Ciber Security’ na ‘Internet of Things (IOT) na kuangalia namna ambavyo teknolojia hizo zitaweza kuisaidia Serikali katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Dkt. Mvulla amefafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha vijana hao wanazielewa teknolojia mpya zinazoibukia na kupata uzoefu na ujuzi wa kutosha wa matumizi sahihi ya teknolojia hizo.

Kwa upande wake Meneja wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), SACP Raphael Rutaihiwa amewakumbusha vijana hao kuzingatia maadili ya utumishi wa umma wakati wote wanapokuwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na mavazi, weledi, uadilifu na nidhamu.

Bi. Glory Baraka, mwanafunzi wa mwaka wa pili (2) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameeleza matarajio yake kuwa ni kujikita katika eneo la Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) na kutumia ujuzi huo katika ushindani wa soko la ajira.

Naye Bw. Frank Mhoja mwanafunzi wa mwaka wa pili (2) Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ameishukuru e-GA kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo ambayo anaamini yatawasaidia kuzielewa teknolojia mpya na kutumia teknolojia hizo katika uvumbuzi wa mifumo mbalimbali itakayosaidia Serikali katika utendaji kazi.

Programu hiyo maalumu ya mafunzo kwa vitendo inahusisha wanafunzi 65 kutoka vyuo kumi na mbili 12 Tanzania bara na Visiwani, mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa wiki 10.