emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

FAHAMU MAKOSA SABA (7) AMBAYO MTUMISHI WA UMMA ANAPASWA KUYAEPUKA KATIKA MATUMIZI YA SERIKALI MTANDAO


FAHAMU MAKOSA SABA (7) AMBAYO MTUMISHI WA UMMA ANAPASWA KUYAEPUKA KATIKA MATUMIZI YA SERIKALI MTANDAO


Serikali Mtandao ni matumizi ya TEHAMA katika utendaji wa kazi Serikalini na utoaji wa huduma kwa wananchi, dhamira kuu ya Serikali Mtandao ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa urahisi na haraka zaidi mahali walipo.

Ili kuhakikisha dhamira ya ujenzi sahihi wa Serikali Mtandao inafikiwa, Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10, Sura Na. 273 ya Mwaka 2019, inatoa muongozo wa namna bora ya matumizi sahihi na salama ya ujenzi wa Serikali Mtandao pamoja na kuainisha makosa ya matumizi ya Serikali Mtandao na adhabu zake kwa watumishi wa umma.

Makosa haya yameainishwa kwa watumishi wa umma kwakuwa, wao haswa ndio watumiaji na watekelezaji wakuu wa Serikali Mtandao ambao hutekeleza majukumu yao kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA na miundombinu yake ili kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kidijitali.

Ikiwa watumishi wa umma watakosa weledi na uzalendo, dhamira ya Serikali Mtandao haiwezi kufikiwa na ndipo Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10, Sura Na. 273 ya Mwaka 2019 kupitia Kifungu cha 57(1), ikabainisha makosa saba (07) ambayo mtumishi wa umma anapaswa kuyaepuka ili kuwa na Serikali Mtandao yenye tija.

Kosa la kwanza (a) kufichua au kushirikisha taarifa za kiofisi au kumbukumbu yoyote ya kielektroniki iliyopatikana wakati wa ajira kwa watu wasiohusika. Mtumishi wa umma hapaswi kufichua au kushirikisha taarifa kutoka ofisi ya umma kwa mtu au makundi sogozi kupitia mitandao ya kijamii kama vile ‘WhatsApp’, ‘Instagram’, ‘Facebook’ n.k ufichuaji na ushirikishaji wa taarifa za Serikali unapaswa kufanywa kwa kufuata utaratibu wa kiofisi ulioainishwa tu na si vinginevyo.

Kosa la pili (b) ni kupakua ‘download’ mafaili yasiyoidhinishwa kwa kutumia vifaa vya kieletroniki vya ofisi kama vile Kompyuta, flash, intaneti n.k. Mfano wa mafaili haya ni filamu au nyimbo za muziki. vifaa vya ofisi vinapaswa kutumika kwa shughuli za kiofisi tu.

Kosa la tatu (c) ni kusambaza ‘disseminate’ au kutuma ‘transmit’ taarifa rasmi au data za serikali kupitia njia zisizoidhinishwa, kwa mujibu wa Mwongozo wa Matumizi Bora, Sahihi na Salama ya Vifaa na Mifumo ya TEHAMA Serikalini wa mwaka 2022 (kipengele na 3.3.8), njia iliyoidhinishwa ya usambazaji wa taarifa za Serikali, ni kupiti Mfumo wa Barua pepe za Serikali (GMS), hivyo kusambaza au kutuma taarifa za Serikali kupitia baruapepe nyingine ni kosa kisheria.

Kosa la nne (d) ni kuzifikia au kupata taarifa au program za Serikali kupitia vifaa vya TEHAMA vya serikali bila idhini. Mtumishi wa umma anayetakiwa kuzifikia taarifa au vifaa hivyo ni yule tu aliyepewa idhini kwa mujibu wa sheria na taratibu za kiofisi. Si kila mtumishi wa umma anapaswa kuzifikia taarifa zote za Serikali bali ni wale tu wanaoruhusiwa na walioidhinishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Kosa la tano (e) ni kosa la kuondoa, kuharibu au kubadili data, kumbukumbu za kielektroniki, mifumo au vifaa vya kielektroniki isivyo halali. Mfano wa kosa hili ni kuharibu kwa nia ovu kompyuta ya ofisi au taarifa muhimu za Serikali, kwa lengo la kupoteza Ushahidi au kwa maslahi binafsi kwa kushirikiana na watu wenye nia ovu.

Kosa la sita (f) ni kushindwa kufuata kwa kujua au kwa uzembe; miongozo ya kiufundi na viwango vilivyowekwa kuhusu masuala ya usalama. Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imeandaa Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao ambayo inapaswa kufuatwa na taasisi zote za umma katika masuala ya usalama wa TEHAMA. hivyo watumishi wa umma wanapaswa kuizingatia miongozo hiyo.

Kosa la saba (g) ni kutofuata taratibu na miongozo iliyowekwa katika uanzishwaji wa miradi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma, miradi yote ya TEHAMA ni lazima ifuate utaratibu kama ilivyoelezewa katika kifungu cha 24 cha sheria hii, na ukiukwaji wa utekelezaji ni kosa kwa mujibu wa sheria hii.

Sheria imeweka wazi adhabu za makosa haya kwa kosa namba 1,3,4 na 6 adhabu yake ni faini isiyo chini ya Shilingi Milioni Tano (5,000,000/-) na isiyozidi Shilingi Milioni Kumi (10,000,000/-) au kifungo kisichopungua miezi sita (6) na kisichozidi miezi 12 au adhabu zote kwa pamoja.

Kwa upande wa kosa namba 2,5 na 7 adhabu yake ni faini isiyo chini ya Shilingi Milioni Tatu (3,000,000/-) na isiyozidi Milioni Tano (5,000,000/-) au kifungo kisichopungua miezi sita (6) na kisichozidi miezi 12 au adhabu zote kwa pamoja.

Kifungu cha 57(2) kimeendelea kubainisha kuwa, Mtumishi wa Umma ambaye atakiuka masharti ya Sheria ya Serikali Mtandao, atastahili hatua za kinidhamu au kijinai kama ilivyoelezwa chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma (sura 298) au sheria nyingine husika. Hatua hizi ni pamoja na kufukuzwa kazini, kuonywa, kupunguzwa cheo, karipio, kupunguzwa mshahara n.k

Sheria hii pia chini ya Kifungu cha 58(1) imetoa adhabu ya jumla kuwa, mtu ambaye atakiuka masharti yoyote ya Sheria hii ambapo adhabu maalum haijatolewa atakua ametenda kosa na atakapotiwa hatiani, basi atastahili kulipa faini isiyopungua shilingi milioni mbili (2,000,000/-) na isiyozidi shilingi milioni ishrini (20,000,000/-) au kifungo cha muda usiopungua miezi sita na isiyozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja kifungo na faini.

Pamoja na adhabu tajwa, Sheria, chini ya kifungu cha 58(2) imeelekeza kuwa, kwa mtu ambaye atatiwa hatiani kwa kosa lolote chini ya Sheria hii, basi mahakama pamoja na kutoa adhabu stahiki, inaweza kumuagiza mtu huyo kulipa kwa Mamlaka kiwango kinacholingana na gharama ya ukarabati wa uharibifu wowote uliosababiswa. Malipo hayo yatakua kama fidia ya uharibifu aliosababisha.

Ili kukuza matumizi ya TEHAMA serikalini, Mamlaka ya serikali Mtandao imeanzishwa kwa lengo la kuhakikisha hilo, na ili kuepusha kukwamishwa kwa namna moja au nyingine sheria imeweka masharti ambayo kila mtumishi wa umma anapaswa kuyaepuka katika matumizi ya Serikali Mtandao, na kushindwa kufuata masharti hayo basi mtumishi huyo atapatiwa adhabu kwa mujibu wa sheria kama ilivotajwa hapo juu.