Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lipo tayari kutumia huduma zinazotolewa na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) ikiwemo kutumia Mfumo wa Barua Pepe wa Serikali (GMS) na kuhifadhi tovuti yao kwa eGA ili kuhakikisha taarifa za baraza hilo zinakuwa mahali salama.
Hayo yamesemwa na Meneja TEHAMA wa Baraza hilo Bw. Isaac Dirawang wakati wa kikao cha pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Wakala kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Mipango Tanzania Februari 05, 2016.
“Tumekuwa tukihifadhi tovuti yetu mahali kwingine lakini baada ya kikao hiki nimegundua kuwa ili mifumo na taarifa za Serikali ziweze kuwa salama ni muhimu kuziweka katika Vituo vya Data ambavyo zitahifadhi taarifa hizo hapahapa nchini na kwakuwa eGA mnatoa huduma hiyo nadhani ni vema kuhamisha tovuti yetu kwenu”, alisema Bw. Dirawang.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Bi. Anna Dominic alisema kupitia uwasilishwaji uliofanyika wameona namna Wakala ilivyokuja kurahisisha kazi na kuongeza ufanisiwa taasisi za umma kwa kutumia TEHAMA.
“Tumefurahi kwa kuwa kikao hiki kimetuongezea uelewa mpana wa namna eGA inavyotekeleza majukumu yake na kwakweli mifumo ambayo mmeitengeneza inatija kwa taasisi na Serikali kwa jumla kwakuwa sasa kila kitu kinaweza kufanywa na taasisi husika kwa kuongeza, kupunguza na kupandisha taarifa mbalimbali kwenye mifumo hiyo kwa manufaa ya wananchi wote”, alieleza Bi. Anna.
Aliongeza kuwa, Serikali Mtandao imekuwa ikitumika katika masuala mbalimbali ya utendaji kazi Serikalini na hivyo kuna umuhimu wa Wakala kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea kila siku ili waweze kutekeleza kazi zao kiufanisi zaidi.
“Awali tulikuwa tukitumia makaratasi kwa wingi lakini kutokana na uwapo wa Serikali Mtandao imepunguza kwa kasi matumizi hayo. Sasa tunaweza kuhariri mtandaoni na kutumia Mfumo wa Barua Pepe ya Serikali katika Mawasiliano”, alisisitiza Bi. Anna.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala Bw. Benedict ndomba, aliwaambia watumishi wa Baraza hilo kuwa Wakala imetengeneza mifumo mingi ambayo imerahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa uhakika kwa wananchi.
“Tovuti Kuu ya Serikali iliyotengenezwa na Wakala imekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi na taasisi za umma kwakuwa taarifa muhimu kama vile sharia zote zinapatikana kiurahisi. Inasikitisha kuona watumiaji wakubwa wa tovuti hiyo ni taasisi binafsi na hivyo basi nawaomba muweze kusoma yaliyomo kwenye tovuti hiyo”, alisema Bw. Ndomba
Aidha, alisema Wakala imetengeneza mfumo wa utoaji huduma kwa simu za mkononi ambapo taasisi za Serikali zinaweza kutumia mfumo huo na kutumia namba *150*00# hadi *150*99# kwa kutuma ujumbe wa makundi kwa wakati mmoja na hivyo wananchi kupata taarifa hizo kwa haraka.
Hadi sasa Baraza hilo linatumia huduma mbalimbali zinazotelewa na Wakala zikiwemo Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS) pamoja na Masafa ya Intaneti ya Serikali