emblem

Mamlaka ya Serikali Mtandao

Uadilifu na Ubunifu kwa Utoaji Huduma Bora kwa Umma
TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

eGA Yawezesha Asasi za Serikali Kutoa Huduma Kwa Simu za Mikononi


eGA Yawezesha Asasi za Serikali Kutoa Huduma Kwa Simu za Mikononi


Mkurugenzi wa Usimamizi wa Huduma za TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) Bw. Benedict Ndomba amesema Wakala imeziwezesha na kutengeneza mifumo ya utoaji huduma kwa njia ya simu za mkononi kwa Wakala wa Usajili na Ufilisi (RITA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha (AUWASA), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.

“Tumetengeneza mifumo hiyo ndani ya mwezi mmoja na tumetumia wataalam wa TEHAMA kutoka taasisi husika chini ya usimamizi wetu kutoka eGA ikiwa ni njia mojawapo ya kuwajengea uwezo wataalam hao”, alifafanua Bw. Ndomba.

Akielezea manufaa ya mfumo huo, mtaalam wa Ubora wa Mifumo na Uhakiki kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bi. Florida Msuya amesema “mfumo utaongeza mauzo ya umeme kwa kuwa mteja ataweza kununua umeme popote alipo na kwa wakati wowote na hata kama likitokea tatizo atapata ujumbe papo hapo”. 

Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha (AUWASA) Bw. Ndaki Tito amesema wameanza kutumia mfumo huo mwezi Machi, 2018 na umewarahisishia wateja wao kupata taarifa mbalimbali zinazohusu huduma ya maji.

“Kwa sasa wateja wetu wanapata taarifa mbalimbali zinazohusu gharama za vifaa kwa ajili ya huduma za kuunganishiwa maji, taarifa zao za malipo , bili za kila mwezi pamoja na malimbikizo ya madai ya mteja kupitia simu zao za mkononi wakati wowote na mahali popote kwa kutumia namba ya msimbo *152*00# na kuchagua huduma wanayoitaka.”, alieleza Bw. Tito.

Ameongeza kuwa, kabla ya kutumia mfumo huo, AUWASA ilikuwa ikitumia gharama kubwa kuwafikia wateja wake na utoaji wa taarifa pia ulikuwa ni mgumu. Lakini kwa sasa, mambo yamerahisishwa na wateja wao wanafurahia huduma kupitia simu zao za mkononi. 

Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa Bw. Jonas Kilima amesema mfumo utazinduliwa mwezi Mei, 2018 na wananchi wajiandae kuutumia kwa kuwa ni njia rahisi ya kupata taarifa na huduma mbailimbali nwanazozitoa.

“Mfumo huu utampunguzia gharama mteja za kufuata huduma kwakuwa atatumia namba *152*00# na hapo atakutana na huduma ananazozitaka. Pia, tutakuwa na hazina data ya wadau wetu wa mkoa ndani ya mfumo hivyo tutawasaidia wadau wengine ambao wataonesha umuhimu wa kukutana na wale wanaowahitaji kama vile wafanyabiashara ili kwa pamoja tulete maendeleo yenye tija”, alisema Bw.Kilima.

Vilevile amesema, sababu ya kutengeneza na kutumia mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya simu ya mkononi ni kutokana na ukweli kwamba kwa sasa wananchi wengi wanatumia simu na hivyo njia pekee ya kuwafikia kwa wakati  ni kwa kutumia simu zao.

Uwezeshaji wa taasisi hizi ni matokeo ya mafunzo yaliyotolewa na Wakala ya Serikali Mtandao kuanzia mwezi Septemba mpaka Novemba 2017 ambapo taasisi za Serikali Sitini na Saba (67) zilishiriki katika mafunzo hayo.